Mradi mkubwa wa umeme Jua Shinyanga kuanza Novemba 2022

 Waziri wa Nishati, Mhe. January Makamba akitazama ramani ya eneo kutakapojengwa mitambo ya umeme jua  itakayozalisha umeme wa kiasi cha megawati katika Kijiji cha Ngunga wilayani Kishapu Mkoa wa Shinyanga. Kulia kwake ni Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Sophia Mjema.

                     ................................

Mradi mkubwa wa uzalishaji umeme kwa kutumia Jua wa kiasi cha megawati 150 utaanza kutekelezwa mwezi Novemba mwaka huu wilayani Kishapu mkoa wa Shinyanga na kuingizwa katika gridi ya Taifa.

Hayo yameelezwa wakati wa ziara ya Waziri wa Nishati, Mhe.January Makamba wilayani Kishapu wakati alipofika katika Kijiji cha Ngunga, kutakapojengwa mitambo ya umeme Jua pamoja na kuzungumza na wananchi katika Kijiji hicho.

 Mradi huo unahusu ujenzi wa kituo cha kuzalisha umeme kwa kutumia jua ambapo gharama ya mradi ni Euro milioni 115.30 sawa na takriban Shilingi bilioni 296.4 na unatarajiwa kukamilika mwaka  2023.

 Mradi unatekelezwa katika awamu mbili ambapo awamu ya kwanza itahusu ujenzi wa kituo cha kuzalisha umeme cha megawati 50 na utekelezaji wa awamu ya kwanza utaenda sambamba na uboreshaji wa miundombinu ya gridi (grid modernization) ili kuruhusu gridi kuweza kubeba umeme wa nishati jadidifu.

Aidha, utekelezaji wa awamu ya pili ya mradi itahusu upanuzi wa kituo cha kuzalisha umeme kwa kuongeza megawati 100.

 Akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Ngunga ambapo mradi huo unatekelezwa, Waziri wa Nishati alisema kuwa “mradi huu sasa utatekelezwa, na tuna uhakika kwa sababu wanaofadhili mradi huu wamepitisha rasmi fedha na sisi tumeshaanza taratibu za kumpata mkandarasi wa ujenzi.

Aliongeza kuwa, taratibu za kumpata mkandarasi zimeshaanza na mpaka sasa  kampuni tatu zimeshachaguliwa ambazo zina uwezo zaidi na kwamba mwisho wa mwezi huu mkandarasi wa mradi huo atapatikana.

“Mradi  huu utabadilisha sura ya Kishapu kwa kuwa, kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi yetu, umeme wa jua utaingia kwenye gridi ya Taifa na sehemu itakayoingiza umeme huo ni Kishapu,  Wilaya hii itakuwa kwenye ramani ya dunia na watu watakuja kuona na kushuhudia mradi huu utakaotumia heka  zaidi ya heka 1000,” alisema Makamba

 Vilevile alisema kuwa, mradi utaambatana na miradi mingine ya kijamii kama maji, umeme vitongojini, shule na zahanati.

Kuhusu fidia za wananchi waliopisha mradi huo,  aliiagiza TANESCO kuhakikisha kuwa kunakuwa na uwazi wa fidia hizo ikiwemo suala la mipaka, kiasi kinacholipwa na kile kinachofidiwa ili kuondoa malalamiko miongoni mwa wananchi kuhisi wamedhulumiwa.

Aliwataka wathamini pia kutenda haki ili kila mwananchi wa kijiji hicho aufurahie mradi huo badala ya kuuona mradi kama chanzo cha dhuluma kwao.

Waziri wa Nishati, January Makamba yupo katika ziara ya kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya nishati, kusikiliza kero za wananchi na kuzitatua pamoja na kuhamasisha matumizia ya nishati safi ya kupikia.


 




 




 



Post a Comment

Previous Post Next Post