Rais Samia awamwagia madola wachezaji Jumuiya ya Madola- Mhe Mchengerwa


Na John Mapepele

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe, Mohamed Mchengerwa  amesema  Serikali inakwenda kutoa zawadi kwa wachezaji wote watakaoleta medali za mashindano ya madola yanayoanza nchini Uingereza hivi karibuni kama hamasa maalum kwa wachezaji.

Amesema kwa mara ya kwanza  kabisa Serikali imeandaa zawadi dola  10000 kwa mshindi atakayerejea na medali ya dhahabu na 
dola 7000 kwa mshindi wa medali ya fedha  na mshindi atakayeshinda  medali ya shaba atapata dola za kimarekani 5000.

Mhe, Mchengerwa ameyasema hayo leo Julai 20, 2022 kwenye hafla ya  kuwaaga wachezaji wa Tanzania wanaokwenda kushiriki mashindano ya Jumuiya ya Madola nchini Uingereza.

Katika hafla hiyo iliyofanyika Ukumbi wa Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam amewataka wachezaji kuweka uzalendo mbele na kuwataka kurudi na medali.

Amefafanua kuwa watambue kwamba dhamira ya Serikali kwa sasa ni kufanya mapinduzi makubwa ambapo amesisitiza kuwa watanzania wamechoka wanataka matokeo chanya katika mashindano haya.

Amesema Serikali imeacha  kutoa fedha kwenye maeneo mengine kama afya, elimu na miundombinu na kuelekeza fedha kwenye michezo ili wachezaji waweze kufanya vizuri.
Ameongeza kuwa Serikali imegharimia  timu hizo kuanzia Februari mwaka huu hivyo hakuna sababu ya timu hizo kutofanya vizuri.

Aidha, amesema  wachezaji lazima kuzingatia nidhamu katika mashindano hayo.

Kwa upande mwingine ameitaka timu ya taifa ya Michezo wa kabaddi inayokwenda kwenye mashindano ya Afrika huko Misri kufanya  vizuri ili kuwa timu ya tatu kuingia kwenye kombe la dunia.

Amewataka kwenda kuliheshimisha taifa kwa kutumia pia michezo hii kutangaza  Royal Tour.
Aidha, ametumia hafla hiyo kuzindua kampeni ya kuwatumia wasanii na wanamichezo inayojulikana  kama Sensabika ili wananchi wajitokeze kwenye sensa itakayofanyika Agosti 23, 2022.

Amesema kabla ya sensa kutakuwa na mchezo wa kukimbizana na ng'ombe.

Aidha amesema kutakuwa na tamasha la michezo, sanaa na utamaduni kwa ajili ya kuhamasisha sensa.

Post a Comment

Previous Post Next Post