PROF.LUOGA AZITAKA BENKI NA TAASISI ZA FEDHA KUPUNGUZA MASHARTI YA RIBA


Gavana wa benki kuu ya Tanzania ,Prof.Florens Luoga akizungumza na waandishi wa habari katika mkutano huo uliofanyika jijini Arusha leo.
Mwenyekiti wa Taifa wa huduma jumuishi za kifedha ,Nangi Massawe akizungumza na waandishi wa habari katika mkutano huo leo jijini Arusha.
………………………………………………
Julieth Laizer  Arusha 
Gavana wa benki kuu ya Tanzania ,Prof.Florens Luoga amezitaka benki na Taasisi za fedha kupunguza masharti ya  riba na gharama za mikopo ili  malengo yaliyowekwa na benki kuu ya Tanzania(BOT) yaweze kutimia .
Ameyasema hayo leo jijini Arusha katika mkutano  wa 10  wa viongozi kutoka bara la Afrika  na nchi mbalimbali wakiwemo magavana wa benki kuu,manaibu na wataalamu ukiwa na lengo la kuhakikisha huduma jumuishi za kifedha zinawafikia wananchi ili kuleta maendeleo katika nchi.
Gavana amesema kuwa, malengo na mikakati iliyowekwa na benki hiyo ni kupunguza gharama za mikopo kwa wahitaji wa mikopo ili iweze kuwanufaisha walengwa ambao wajasiriamali,hivyo wanafuatilia na kujadili endapo mikakati hiyo imefikiwa .
Amesema kuwa,wanataka kuhakikisha huduma za kibenki zimewafikia wananchi wote ikiwa ni pamoja na  kuhakikisha benki na Taasisi za fedha  zote zimepunguza masharti ya riba ili huduma hizo ziweze kuwanufaisha  wananchi.
Ameongeza kuwa, malengo makuu ya benki hiyo ni kuhakikisha huduma jumuishi za kibenki  zinawafikia wananchi wote huku wakihakikisha benki pamoja na huduma za kifedha  zinapeleka huduma hizo kila mahali.
“pamoja na kujiwekea mikakati hiyo bado kuna changamoto mbalimbali kwani kuna maeneo ambayo hayajafikiwa na huduma hizo mpaka sasa ,hivyo juhudi zaidi zinaendelea kufanyika kuhakikisha huduma hizo zimesambaa kila mahali ili wananchi wote ambao ndio walengwa waweze kufikiwa Kwa haraka “amesema.
Aidha Gavana  amesema kuwa ,serikali imejipanga kuhakikisha kuwa huduma mtandao  zinawafikia wananchi wote ambapo wanataka kuhakikisha kila mwananchi akitembea kilometa tano akutane na huduma .
Naye Mwenyekiti wa Taifa wa huduma jumuishi za kifedha,Nangi Massawe amesema kuwa,bado elimu zaidi inatakiwa kutolewa kuhusiana na maswala ya kifedha ambapo serikali imejipanga kuhakikisha elimu zaidi inaendelea kutolewa hususani  Kwa wanawake.
Amesema kuwa, hadi sasa  asilimia 60 ya wanawake wamefikiwa na huduma za kifedha ambapo mkakati uliowekwa na serikali ni kuhakikisha wanafikia kwa  asilimia 73 hadi ifikapo 2022.
Amesema kuwa, wanaongea na mabenki kuhakikisha wanatoa mikopo ambayo itawawezesha wanawake wenye biashara ndogondogo kuweza kukopa kwenye mabenki na kupata fedha nyingi .
Kwa upande wake Mwenyekiti wa kamati ya maswala ya huduma jumuishi za fedha ,Beng’i Issa amesema kuwa,wamejiwekea mkakati wa kuhakikisha  elimu  ya fedha kwa  wanawake  inawafikia kwa karibu na kuweza kunufaika kwa kiwango cha juu na hivyo kujikwamua kiuchumi.

Post a Comment

Previous Post Next Post