NAIBU WAZIRI KASEKENYA AKAGUA ATHARI ZA MIUNDOMBINU YA BARABARA SONGWE

 

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya (aliyevaa kofia nyeusi) akitoa maelekezo kwa Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) mkoa wa Songwe, Mhandisi  Suleiman Bishanga, alipotembelea na kukagua barabara inayounganisha kata ya Isongole,Ibungu, Katengele,Lubanda kwenda Keikei, zilizopo wilaya ya Ileje, mkoani humo.

Baadhi ya Vijana wakitengeneza barabara ya dharula kwa ajili ya kupitisha magari kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha katika kata ya Isongole na kuharibu miundombinu ya barabara,mkoani Songwe.

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, akizungumza na Wananchi wa  kata ya Sange, Wilayani Ileje, mkoani Songwe, mara baada ya kukagua miundombinu ya barabara iliyoharibika kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha Wilayani humo.

                         ...........................

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, amekagua athari zilizotokana na mvua hizo kwenye miundombinu ya barabara hiyo  ambayo imeharibika kufuatia magema kuporomoka  barabarani na kusababisha kufunga kwa barabara.

“Barabara hii inaunganisha wilaya ya ileje na wilaya ya Rugwe, na ndiyo barabara muhimu kwa mawasiliano baina ya Mikoa ya Songwe na Mbeya na eneo ambalo barabara hizi zimeharibika ni maeneo ya miinuko na kuna  maporomoko mengi sana kutokana na asili ya udongo wa eneo hili hasa katika kipindi cha mvua,”amefafanua Mhandisi Kasekenya.

Amesema kuwa Serikali itahakikisha maeneo yote yaliyopata athari za mvua yanarekebishwa kwa haraka ili shughuli za kibinadamu ziweze kurejea.

Aidha, Mhandisi kasekenya ametoa pole kwa familia zilizopata na maafa ikiwepo ya vifo vya wananchi watano, nyumba kubomoka, mazao kuharibika pamoja na mifugo kufa kutokana na kuporomokewa na udongo.

“Tunatoa pole kwa wananchi wote wa Wilaya ya Ileje na  vijiji vya Sange na kisesi, kwa kuwapoteza ndugu zao waliofariki pamoja na wengine waliopoteza mifugo, na mazao yao kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha wilayani,”amesema Mhandisi Kasekenya.

Naye Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Songwe Mhandisi Suleimani Bishanga, amemhakikishia Naibu Waziri Kasekenya ndani ya wiki moja barabara na madaraja yaliyopata athari yataimarishwa na kuendelea kutumika.

Kwa upande wa wananchi wa wilaya ya ileje, wameiomba Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kuweza kuwasaidia kufungua barabara na madaraja yaliyoharibika kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha wilayani humo ili waweze kuendelea na shughuli zao za kibinadamu


Post a Comment

Previous Post Next Post