SIKU YA KWANZA KUELEKEA KILELE CHA MAADHIMISHO SIKU YA URITHI WA DUNIA - AFRIKA YAANZA KWA KISHINDO KILWA MASOKO

 Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania - TAWA Leo tarehe 04/05/2022 imeanza rasmi maadhimisho ya Siku ya Urithi wa Dunia - Afrika ambayo kitaifa yanafanyika katika Mji wa Kilwa Masoko wilaya ya Kilwa Mkoani Lindi


Ikiwa ni siku ya kwanza kuelekea kilele cha maadhimisho hayo, TAWA imeratibu na kushiriki katika shughuli mbalimbali za kiuhifadhi na kijamii ikiwemo michezo kwa Kushirikiana na wakazi wa Mji wa Kilwa Masoko na wengine kutoka Mikoa ya Jirani hususan Mkoa wa Dar es Salaam.

Akizungumza katika ufunguzi wa shughuli zilizofanyika katika siku ya kwanza ya maadhimisho hayo, Kaimu Naibu Kamishna wa TAWA Sylivester Mushi amesema kupitia maadhimisho hayo TAWA inatarijia wananchi wa Kilwa Masoko kuhamasika katika kutangaza Utalii

Kwa upande wake, Kamishna Msaidizi Mwandamizi - Kanda ya Mashariki Abraham Jullu amesema kupitia Royal Tour iliyozinduliwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan TAWA imejiandaa na Iko tayari kupokea wageni wengi.

Mashindano ya kuendesha mitumbwi ya asili ni mojawapo ya matukio yaliyokuwa na mvuto mkubwa na kuibua hisia za watu wengi katika Mji wa Kilwa Masoko siku ya leo, ambapo wakazi wa Mji huo walishiriki katika mashindano hayo yaliyoratibiwa na TAWA

Aidha, upandaji wa mikoko katika eneo la Kilwa Kisiwani pamoja na kutembelea vivutio vilivyopo katika Hifadhi ya Eneo la Urithi wa Dunia la Kilwa Kisiwani na Songo Mnara ni miongoni mwa shughuli zilizofanyika siku hii.

Hali kadhalika, Michezo ya wavu na kukimbia mchamchaka ni miongoni mwa shughuli zilizofanyika siku hii ambapo jumla ya "Jogging Clubs" nne (4) zilishiriki zikiwemo Kilwa Masoko Jogging, Kilwa Green, EFM "Jogging Club" ya Dar es Salaam na TAWA "Jogging Club".

Kilele Cha Maadhimisho ya Siku ya Urithi wa Dunia - Afrika kitafanyika kesho tarehe 05/05/2022 katika kiwanja Cha Mkapa Garden ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Lindi Mhe. Zainab Telack



Post a Comment

Previous Post Next Post