KOMBE LA DUNIA KUTUA TANZANIA MEI 31 MWAKA HUU, RAIS SAMIA MGENI RASMI


Na John Mapepele

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mhe, Samia Suluhu Hassan anatarajia kuwa mgeni rasmi kulipokea Kombe la Dunia kwenye ziara yake nchini Mei 31, 2022 kwa  niaba ya watanzania  wote ikiwa ni mkakati maalum wa kuitangaza Tanzania na kuwataka watanzania  kujitokeza  kwa wingi Juni 1, 2022 Uwanja  wa Taifa Jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuliona na kupiga picha.

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe, Mohamed Mchengerwa amesema haya leo Mei 5, 2022 kwenye uzinduzi wa ziara ya Kombe hilo nchini,  jijini Dar es Salaam ambapo amepiga mpira na kufunga penati kwenye goli la mfano na  kuashiria ufunguzi rasmi wa ziara ya ujio wa kombe hilo nchini.

Amesema  ujio wa  kombe hilo unaonyesha  jinsi Shirikisho ya Mpira wa Miguu Duniani (FIFA) linavyotambua jitihada kubwa zinazofanywa  na Tanzania kwenye michezo katika kipindi hiki.

Aidha, amesema  Serikali ya Awamu ya Sita  inayoongozwa na Rais Samia  imefanya mapinduzi makubwa kwenye michezo   katika kipindi kifupi kwa  kuwa  inaamini  kuwa michezo ni biashara inayozalisha ajira kubwa  na kwamba inachochea   uchumi wa nchi kwa ujumla.

Ameongeza kwamba katika  kuendelea kuitangaza Tanzania kimataifa  Serikali  katika kipindi hiki imeridhia kuratibu na kufadhili  Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Soka Barani Afrika utakaofanyika jijini   Arusha ambao utahudhuriwa  na zaidi ya nchi  54 pamoja  na viongozi wakuu wa mashirikisho  na vyama  vikuu   vya michezo akiwemo Rais wa FIFA.

Amesema mkutano huo  unafanyika  jijini Arusha eneo ambalo ni kitovu cha utalii nchini,   jambo ambalo litasaidia kufungua  milango ya   kutangaza  vivutio mbalimbali vya utalii   kwa wageni  watakaoshiriki kwenye mkutano huo.

Kwa  upande mwingine,  amesema  Serikali  imedhamiria  kuandaa miundombinu ya kisasa ya michezo  ili kuweza  kuratibu mashindano ya  Kombe la Mataifa ya Afrika hapa nchini ambapo ameiomba Kampuni ya   Coca Cola kujitokeza  kushirikiana  na Serikali kujenga  viwanja vitakaokidhi mataka ya  kufanya  mashindano hayo ya kimataifa.

“Natambua mchango wenu katika michezo na  kuitangaza  Tanzania kwa ujumla  nipende kutumia  fursa hii kuwaomba Coca Cola kushiriki  kikamilifu  kwenye ujenzi huo. Tunahitaji viwanja  vitatu  ili tuweze kuandaa mashindano haya” amefafanua Mhe. Mchengerwa.

Amemwagiza Mkurugenzi wa Michezo nchini, Yusufu Singo kuhakikisha Wizara inashirikiana na Coca Cola   kutengeneza mfumo wa matangazo kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa utakaokuwa  ukikodishwa kurusha  matangazo kwa makampuni mbalimbali.   

Pia ameagiza Idara ya Michezo, Baraza la Michezo la Taifa (BMT) na Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF)  kuwatafuta wachezaji watanzania wanaocheza  katika  timu za kubwa  duniani ili kuunda timu  bora ya taifa itakayoweza kufanya vizuri  zaidi kwenye  mashindano ya kimataifa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Coca Cola Kwanza Tanzania, Unguu Sulay, Kampuni ambayo inadhamini ziara ya ujio wa Kombe hilo nchini amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi chache zilizopewa heshima ya kutembelewa na Kombe hilo na kuahidi kufanya kazi kwa karibu na wizara.

Rais wa TFF, Wallace Karia ameipongeza Serikali kwa juhudi za kufanya maboresho kwenye sekta za michezo nchi huku akifafanua kuwa Wizara imekuwa ikifanya kazi kwa karibu sana na wadau  kuliko awali hali inayopelekea kuanza kufanya  vizuri kwenye michezo.



Post a Comment

Previous Post Next Post