NA: EBEN-EZERY MENDE
KARIBU katika safu ya Elimu ambayo imelenga kukuhabarisha, kukufafanulia na kuyachambua kwa kina masuala yanayoihusu elimu ya nchi yetu, Tanzania.
Kutokana na umuhimu wa elimu kwa jamii yoyote safu hii itajitahidi kuhakikisha inakupa ladha ya elimu, changamoto, mikakati iliyopangwa, namna wadau wa elimu wanavyoshauri na matarajio ya Watanzania kuihusu elimu.
Ipi njia bora ya kupita ili kuwafikisha wanafunzi katika uhitimu wa elimu ambayo itabeba mambo mawili la kwanza likiwa ni kumudu kujiajiri na pili ni elimu hiyo inawezaje kumsaidia kupata soko la taaluma aliyoisoma ndani na nchi ya nchi.
Safu hii ni mlango wa kufungua mijadala ya elimu na kwa kuanzia lipo swali linalohoji, Je ni muda gani sahihi ambao ukishapita ni muafaka kufanyika mabadiliko ya mtaala na mfumo wote wa kujifunza na kufundisha?
Swali hili linatokana na mfumo uliopo sasa ambao hauna ratiba ya kufanya utafiti na kukusanya maoni ya wadau wa elimu kabla ya viongozi wa kisiasa kufanya uamuzi na kuanza kutekelezwa bila ushirikishwaji wa jamii.
Hili limekuwa jambo la kawaida kwamba mwaka huu wa 2022 vitabu vya kiada na ziada vikawa ni tofauti na vilivyotumika mwaka jana 2021 na bila hofu mwaka kesho 2023 yawezekana vitabu vikawa tofauti na vilivyotumika mwaka huu.
Hapo ndipo penye shina la swali la safu hii kwamba mfumo wetu wa elimu ya Tanzania ueleze wazi kwamba ili kubadilisha mfumo na vitendea kazi kuwe na muda maalumu na si kiongozi yeyote wa kisiasa anapokasimishwa madaraka kwenye sekta ya elimu anafanya uamuzi hata wa kutengua mipango iliyofanyiwa utafiti inayoanza kutekelezwa.
Pamoja na jitihada za Serikali kujenga majengo mazuri ya madarasa na vyoo vya wanafunzi bado ipo changamoto kubwa ya uwiano wa walimu katika shule za msingi na sekondari.
Kupitia vyombo vya habari hivi karibuni tumesikia shule kadhaa nchini kukabiliwa na changamoto ya matundu ya vyoo.
Changamoto hiyo imeonekana kuwa kubwa hasa kwa wanafunzi wenye uhitaji maalumu ambapo imeripotiwa wanafunzi 37 wenye mahitaji maalumu wa Shule ya Msingi Igunga wanakabiliwa na shida ya kukosekana matundu ya vyoo maalumu kwa ajili yao.
Hata hivyo madarasa yenye sura nzuri na vyoo vimeonekana kongole kwa hatua hiyo lakini kilichofanyika ni kumhamisha mtoto kutoka kujifunza chini ya mti na kuingia darasani lakini elimu ni zaidi ya madarasa na vyoo.
Baada ya mwanafunzi kuhitimu anapoingia sokoni kutafuta ajira aliyesomea chini ya mti akiwa na vitabu toshelevu, daftari na waalimu wa kulingana na idadi inayoshauriwa ya wanafunzi 30 hadi 45 kwa mwalimu mmoja na atakayesoma akiwa ndani ya darasa zuri lisilo na walimu toshelevu yupi atakaemshinda mwenzake sokoni?
Kipi kitambulisho cha kumbaini mwanafunzi aliyesomea chini ya mti na aliyesomea ndani ya darasa zuri baada ya kuhitimu mafunzo?
Hivi karibuni tumemsikia Mbunge wa Ubungo, Profesa Kitila Mkumbo akitoa hoja bungeni kuhusu hali ya elimu ya Tanzania kwamba haiko sawa kwani hailengi kumsaidia mwanafunzi kujimudu bali kuwa tegemezi.
Hoja hiyo imepokelewa na kuungwa mkono na wabunge wengi bungeni wakijaribu kuonesha kwamba pamoja na mambo mengine lugha imekuwa kikwazo cha wanafunzi kuelewa wanachofundishwa lakini pia kwa kutokujua huko pia inawachelewesha kuwa wabunifu wa yale wanayojifunza.
Haya maoni kwa nini yanakuwa na ugumu wa kuyatekeleza wakati tafiti zilizofanyika zimebainisha wazi kwamba nchi zilizoendelea haraka duniani na zilizo kwenye uchumi mkubwa ni zile zilizozingatia kufundisha kwa lugha ya taifa hilo.
Kwa nini hadi leo kuna kigugumizi cha kutekelezwa kwa mfumo wa elimu ya Tanzania ifundishwe kwa lugha ya Kishwahili kuanzia elimu ya awali hadi chuo kikuu?
Hii ikimaanisha Kiswahili iwe lugha ya kujifunzia na kufundishia na Kiingereza, Kifaransa, Kiarabu, Kichina na nyinginezo ziwe somo la kujifunza.
Mpango huu uneshajadiliwa mara *chungu tele* bungeni lakini inapofikia hitimisho inabaki kwamba wadau watashirikishwa likirudi tena kukusanya maoni linaanza upya na mwisho imebaki kitendaliwi.
Upo upotofu wa fikra kwamba mtu anaejua kuzungumza Kiingereza pengine na kifaransa au Kijapani mtu huyo ana uelewa mpana wa mambo mengi ya tofauti jambo ambalo si kweli.
Hizo ni lugha tu kama ambavyo Mtanzania yeyote anaweza akaifahamu kwa ufasaha lugha ya kabila la Wachaga, Wahaya, Wangoni, Wapare, Wahehe, Waluguru, Wamakonde, Wamakua, Wayao ama Wamatumbi lakini si kweli kwamba ana utambuzi mpana katika mambo tofauti yaliyo nje ya lugha hizo anazozifahamu.
Tafiti zimebainisha kwamba mtu akifundishwa taaluma yoyote kwa lugha ya malezi (lugha aliyokuzwa nayo) anaelewa vizuri na mapema kuliko mtu anayefundishwa kwa lugha tofauti na ile aliyojifunza kuanza kuongea.
Si hilo tu bali tafiti zimeeleza kwamba mtu anapotaka kujieleza mbele za watu anakuwa huru na kuwasilisha vizuri hoja yake endapo atatumia lugha aliyokuzwa nayo na si lugha mpya aliyoanza kujifunza alipoanza shule.
Naomba kupitia safu hii tujikumbushe kwamba lugha ni bidhaa, lugha ni silaha, lugha ni biashara, lugha ni mali hivyo katika uga wa elimu lugha inapaswa kuzingatiwa vinginevyo tunachechemea kwenye vyote hivyo kwa kutozingatia usahihi wa elimu na matumizi ya lugha.
Nani mwenye utimamu wa fikra anatamani kusifiwa kuwa ni wa taifa fulani kwa kuijua vizuri lugha ya taifa hilo na kuificha lugha yake kwenye begi lakini akiwa amevaa vazi linalomtambulisha uhalisia wa taifa tofauti na analoliwakilisha kwa lugha?
Itawezekana Mmakonde atamani kuitwa Mfipa kwa lugha lakini uhalisia wa chale awe nao kwenye mwili wake.?
Tanzania nchi yenye tunu lukuki ikiwemo ya lugha adhimu ya Kiswahili inatakiwa ionekane kwenye elimu yetu kwa kuwa anaepaswa kujivunia lugha ni mmiliki wake na si mgeni.
Ashakum haikuwahi kuwa tusi hivyo umbumbumbu wa kuidharau lugha ya Kiswahili katika mukhtadha wa lugha rasmi ya kufundishia, lugha rasmi ya matumizi ya kiofisi ufutike na tuithamini ili kujenga ufahamu wa yatokanayo na elimu.
Wajibu wangu ni kuhakikisha kilicho sahihi katika kukuza elimu yetu, kushauri na kukosoa pale panapoonekana panahitaji kufanyika hilo.
Elimu yetu itokanayo na lugha yetu ndani ya nchi yetu ndiyo mafanikio yetu.
0713977600
mendemyself