DARAJA JIPYA LA WAMI KUWEKA HISTORIA YA KWANZA KUKAMILIKA MAPEMA ZAIDI

 


Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, akiwa na Balozi wa Jamhuri ya Watu wa China nchini Tanzania, Mheshimiwa Balozi Mingjian Chen, wakiwasili mkoani Pwani kwa ajili ya kushuhudia utekelezaji wa ujenzi wa Daraja jipya la Wami (m 513.5), ambao umefikia asilimia 77.

Mwakilishi wa Msimamizi wa mradi wa Daraja jipya la Wami (m 513.5), Young Cheol Cheon, akitoa maelezo kwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, wakati akikagua utekelezaji wake, mkoani Pwani.

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, akifafanua jambo kwa Balozi wa Jamhuri ya Watu wa China nchini Tanzania, Mheshimiwa Balozi Mingjian Chen, kuhusu ujenzi wa Daraja jipya la Wami (m 513.5), ambapo sehemu ya kupita magari imemalizika kuunganishwa, mkoani Pwani.

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, akiwa na Balozi wa Jamhuri ya Watu wa China nchini Tanzania, Mheshimiwa Balozi Mingjian Chen, wakikagua sehemu ya kupita magari (deck), iliyokamilika kuunganishwa katika Daraja jipya la Wami lenye urefu wa mita 513.5, mkoani Pwani.

Muonekano wa hatua za ujenzi wa Daraja jipya la Wami lenye urefu wa mita 513.5 na barabara za maingilio zenye urefu wa kilometa 3.8 mkoani Pwani ambapo ujenzi wake umefikia asilimia 77

…………………………………………..

Serikali imesema ujenzi wa Daraja jipya la Wami lenye urefu wa mita 513.5 na barabara za maingilio (km 3.8), unatarajiwa kuandika historia mpya kwa sekta ya Ujenzi mradi kukamilika kabla ya muda uliopangwa kwenye mkataba. 

Ujenzi huu ulioanza mwezi Oktoba, 2018 unatarajiwa kukamilika mapema ifikapo mwezi Julai, 2022 badala ya mwezi Novemba kama ilivyo kwa mujibu wa mkataba wake. 

Hayo yamesemwa na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, wakati akishuhudia ukamilikaji wa sehemu ya kupita magari (deck) kwenye daraja hilo jipya ambalo ujenzi wake umefikia asilimia 77. 

“Hii ni hatua kubwa sana kwa Daraja la aina hii, nimejionea linaendelea vizuri na naamini kutokana na kasi aliyonayo mkandarasi kwa hakika daraja hili litakamilika kabla ya muda”, amesema Prof. Mbarawa. 

Prof. Mbarawa amefafanua ongezeko la magari katika Daraja la Wami la zamani na wembamba wa daraja hilo umesababisha Serikali kujenga daraja kubwa litakaloruhusu magari mawili kupita kwa wakati mmoja na hivyo kupunguza Ajali zilizokuwa zikitokea Darajani hapo. 

Aidha, Prof. Mbarawa amemtaka mkandarasi kuongeza kasi na kuhakikisha anakamilisha kazi zilizobakia ndani ya muda uliopangwa kwa kufanya kazi usiku na mchana pia kuongeza rasilimali watu na mitambo. 

Waziri Prof. Mbarawa ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuendelea kutoa fedha kwa miradi mikubwa inayoendelea ili iweze kukamilika kwa wakati. 

“Serikali itaendelea kuwalipa Mkandarasi na Mhandisi Mshauri kulingana na madai yanayowasilishwa na kuthibitishwa”, amesisitiza Waziri Prof. Mbarawa. 

Kwa upande wake Balozi wa Jamhuri ya Watu wa China nchini Tanzania, Mheshimiwa Balozi Mingjian Chen, ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuendelea kuziamini kampuni za kichina katika utekelezaji wa miradi mikubwa inayoendelea na amefurahishwa kuona kuwa miradi hiyo imekuwa ikitoa fursa kwa wazawa kupata mafunzo wakati wa utekelezaji wa miradi hiyo. 

“Mradi huu umeajiri zaidi ya Watanzania 400 ambao bila shaka wamepata ujuzi mkubwa na itasaidia kukuza uchumi wa ndani”, amesisitiza Balozi Chen. 

Awali akitoa taarifa ya mradi Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), Eng. Rogatius Mativila, ameeleza kuwa ujenzi wa Daraja Jipya la Wami unagharamiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa asilimia 100 kwa jumla ya Shilingi Bilioni 75.13. 

Amebainisha gharama hizo ambazo zinahusisha gharama za ujenzi ni Shilingi Bilioni 67.779, gharama za usimamizi wa Ujenzi ni Shilingi Bilioni 6.307, Gharama za kazi ya Usanifu ni Shilingi Milioni 852.991 na fidia kwa wananchi ni Shilingi Milioni 194.718 .

Eng.Mativila ameongeza kuwa mradi huo umetoa jumla ya ajira 420, kati ya hizo ajira 395 zimetolewa kwa watanzania na ajira 25 ni za wageni.

 

“Ni matarajio yangu kuwa Watanzania wataalamu waliopata ajira na mafunzo kwenye Mradi huu watasaidia kuongeza ujuzi kwa wajenzi na wasimamizi wetu wa ndani ili hatimaye tuweze kutekeleza miradi kama huu kwa kutumia Makandarasi wetu wa ndani”, amesisitiza Mativila.

Ujenzi wa Daraja Jipya la Wami una lengo la kutatua changamoto zilizokuwepo katika Daraja la zamani kutokana na kutokidhi mahitaji ya watumiaji wa daraja hilo tangu lilipojengwa Mwaka 1959.


Post a Comment

Previous Post Next Post