Na. John Mapepele
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe Mohamed Mchengerwa amewatoa hofu mashabiki wa soka wanaotaka kwenda Afrika Kusini kuishangilia Timu ya Simba katika mchezo wa raundi ya pili robo fainali ya Mashindano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika kuwa watakuwa salama.
Mhe. Mchengerwa ametoa kauli hiyo leo Aprili 21, 2022 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam alipokuwa akiongea na Vyombo vya Habari.
"Niseme tu kwamba sisi kama Serikali tunafuatilia kwa karibu usalama wa timu na hivi ninavyoongea nimemteua Msaidizi wangu Mkurugenzi wa Michezo ili aweze kuniwakilisha kusimamia hili" amefafanua Mhe. Mchengerwa
Aidha, Mhe. Mchengerwa amesema watanzania na waafrika Kusini ni ndugu wa muda mrefu hivyo ni mategemeo kuwa hakutakuwa na jambo lolote linaloweza kuhatarisha usalama.
Ameeleza kuwa katika mechi hiyo Timu ya Simba inakwenda kushindana siyo kushiriki ili kuliwakilisha taifa ambapo amewataka wachezaji kucheza kwa weledi na ari kubwa ili ipige hatua katika hatua inayofuata hatimaye irudishe kombe nyumbani.
Akizungumzia kuhusu kuzisaidia timu za taifa, Mhe. Mchengerwa tayari Serikali imeshatoa fedha kwa ajili ya kufanya maandalizi kwenye makambi yote ya timu hizo.
Pia, amesema dhamira ya taifa ni kushiriki kwenye Mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) na kuratibu mashindano hayo hapa hapa nchini.
Amesema tayari Serikali inafanya maandalizi hayo kwa kuandaa timu bora zitakazofuzu na kuandaa miundombinu ya michezo hiyo.
Katika hatua nyingine Mhe. Mchengerwa amesema kutokana na kuendelea kufanya vizuri, Tanzania imekuwa miongoni mwa nchi nane Afrika ambazo kombe la dunia litapita ambapo hapa nchini linatarajia kufika mwisho wa mwazi huu.