Na John Mapepele
Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara. Mhe, Abdulrahman Kinana leo Aprili 20, 2022 ametembelea Ofisi za Programu ya Urithi wa Ukombozi wa Bara la Afrika jijini Dar es Salaam na kupongeza juhudi kubwa zinazofanywa na Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo baada ya kupata maelezo ya Waziri anayeisimamia Wizara hiyo, Mhe. Mohamed Mchengerwa.
Mhe. Kinana amesema Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo ndiyo uti wa mgongo wa taifa lolote na kusifu jitihada zinazofanywa na Wizara kwenye kuhakikisha utamaduni wa kiukombozi wa Bara la Afrika unaenziwa na kuhifadhiwa kwa faida ya sasa na vizazi vijavyo.
Kwa upande wake, Waziri Mchengerwa amefafanua kuwa mpango wa Serikali kwa sasa ni kujenga makumbusho kubwa ya kisasa.
Aidha, amesema programu inaendelea na kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii kukamilisha mchakato wa kuyatangaza maeneo15 ya Urithi wa Ukombozi wa Bara la Afrika yaliyopo nchini kuwa Urithi wa Taifa kwa kuyatangaza kwenye gazeti ya Serikali ili yalindwe kisheria.
Mhe. Mchengerwa amesema Programu hii pia inayomajukumu mengi lakini kubwa zaidi ni kuhakikisha ina enzi, kulinda, kuendeleza, kuhifadhi na kutangaza urithi wa ukombozi wa Bara la Afrika uliopo nchini na Afrika kwa ujumla.
Ameongeza kuwa kutokana na jukumu hili ambalo Tanzania imekabidhiwa hivyo ina wajibu wa kuukumbusha umma wa Afrika kuhifadhi tunu hizi muhimu ili vizazi vijavyo vitambue waafrika ni ndugu na wanaoishi katika misingi hiyo tangu kipindi cha ukoloni hadi kupatikana kwa uhuru wao.