TFRA yaanisha mikakati kuhakikisha wakulima wanapata mbolea

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi inayosimamia Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) Prof. Anthony Mshandete ameweka wazi mikakati mahususi ya kuhakikisha wakulima nchini wanapata mbolea bora kwa ajili ya matumizi ya kilimo.

 Ameeleza mikakati hiyo jana tarehe 29 Aprili, 2022  ambapo wajumbe wa Bodi ya TFRA pamoja na watendaji wa mamlaka hiyo walitembelea eneo kinapojengwa kiwanda hicho  kwa lengo la  kujionea hatua na maendeleo ya ujenzi wa kiwanda kinachotarajia kuanza uzalishaji wa tani 6000 za mbolea mwezi Julai 2022.

 Akieleza mikakati hiyo, Prof. Mshandete alisema mkakati wa kwanza ni kuhakisha mbolea inayozalishwa inakuwa na ubora na viwango vinavyokubalika nchini. Alisema wananchi wakiona ubora wa mbolea inayozalishwa na kiwanda hicho itakuwa rahisi kwa kiwanda kujitangaza na mbolea itauzika  kiurahisi.

 Akielezea mkakati wa pili Prof. Mshandete alisema ni uongozi wa kiwanda kuwa na mkakati wa mawasiliano kwa ajili ya kutangaza aina ya mbolea itakayokuwa ikizalishwa na kiwanda hicho yenye mchanganyiko wa samadi na madini mengine kama phosphate na chokaa tofauti na aina zilizozoeleka kwa wakulima nchini.

 Prof. Mshandete alisema kutokana na ukweli kwamba mbolea inayozalishwa kiwandani hapo kuwa mpya kwenye soko la ndani elimu kuhusu ubora wa mbolea hiyo unapaswa kutolewa ili wananchi waweze kuifahamu na kuwa na utayari wa kuitumia na hivyo kupunguza changamoto ya upatikanaji wa mbolea nchini.

 Aidha, Prof. Mshandete amewataka wasimamizi wa kiwanda cha Itracom Fertilizer LTD kuwa na hari (aggressiveness) katika kutangaza bidhaa na kuwashauri kushiriki katika maadhimisho ya siku ya mbolea yanayotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu ili kuwapa fursa ya kuitangaza bidhaa hiyo.

 Akizungumzia suala la upatikanaji wa malighafi kwa ajili ya uzalishaji wa mbolea  kiwandani hapo Prof. Mshandete alisema  kutatokana na namna nzuri ya kutangaza uwepo wa kiwanda hicho pamoja na kutangaza malighafi zinazotumika katika uzalishaji kutakakofanywa na mwekezaji huyo.

 Pamoja na hayo Prof. Mshandete ametoa wito kwa mwekezaji Itracom Fertilizer LTD kutosita kuishirikisha TFRA na mamlaka nyingine za serikali pindi wanapokutana na changamoto wakati wa utekelezaji wa mradi huo.

 Akizungumza kwa upande wa mwekezaji, Dr. Ntukamazina  Nepomuscene Mkurugenzi wa Utafiti na Ubunifu wa Itracom  Fertilizer LTD alisema ujenzi wa  kiwanda upo katika  hatua nzuri ambapo mitambo imeshaanza kufungwa tayari kuanza uzalishaji ifikapo Julai 2022.

 Aliongeza kuwa, tayari kiasi kikubwa cha samadi kimepatikana na kimefikishwa kiwandani hapo kwa ajili ya kuanza uzalishaji wa mbolea hiyo.

 Uwekezaji huo utakaogharimu kiasi cha dola za kimarekani Milioni 180  ni matokeo ya ziara ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan nchini Burundi na kueleza fursa za uwekezaji zilizopo nchini na kumpata mwekezaji wa kiwanda cha Itracom Fertilizers Limited.




Post a Comment

Previous Post Next Post