Na John Mapepele
Mamia ya wananchi wa Jimbo la Rufiji leo Aprili 29,2022 wamefanya dua maalum ya kumwombea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mhe Samia Suluhu kwenye futari maalum iliyoandaliwa na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo na Mbunge wa Jimbo la Rufiji Mhe. Mohamed Mchengerwa katika eneo la Ikwiriri Wilayani Rufiji.
Dua hiyo maalum imeongozwa na Shehe Athmani Shabani Bofu kutoka Utete akishirikiana na mashehe mbalimbali wa Mkoa wa Pwani ambapo wamemwombea kwa Mwenyezi Mungu, Mhe. Rais Samia afya njema na ufanisi kwenye kazi zake za kila siku.
Akiongea kwenye tukio hilo Mhe. Mchengerwa amemshukuru na kumpongeza Mhe. Rais kwa kazi kubwa anayowafanyia wananchi wa Tanzania ikiwa ni pamoja na wananchi wa Rufiji.
Amesema wananchi wa Rufiji wamenufaika kwa kiasi kikubwa na Maendeleo yanayoletwa na Serikali na kuwataka kuendelea kushirikiana na Serikali yao ili kujiletea maendeleo zaidi.
Ametaja baadhi ya maendeleo kuwa ni pamoja na kuunganishiwa umeme kwa kata zote, kujengewa shule ikiwa ni pamoja na shule maalum ya Bibi Titi Mohamed, madaraja na barabara.
Aidha, amewausia wananchi wa Rufiji kuendelea kumcha Mwenyezi Mungu katika kipindi hiki cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani na baada ya mwezi ambapo amesisitiza kuwa Mwenyezi mungu amempa mwanadau uhai ili amwabudu na kufanya matendo mema.
Katika hatua nyingine Mhe. Mchengerwa amewataka wananchi wa Rufiji kujitokeza kushiriki kwenye sensa itakayofanyika mwaka huu ili Serikali iweze kutambua idadi ya wananchi wake kwa ajili ya kupanga mipango mbalimbali ya maendeleo.