Mhe Gekul awataka watanzania kutumia fursa za Royal Tour


Na. John Mapepele

Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Pauline Philipo Gekul (Mb) amewataka watanzania  kutumia  fursa iliyotengenezwa  na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe Samia Suluhu Hassan   kwenye Filamu ya Royal Tour.

Mhe. Gekul ameyasema  haya leo Aprili 29, 2022 kwenye  semina ya wadau wa sekta ya filamu ya Royal Tour katika ukumbi wa mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere Dar es Salaam.

Naibu  Waziri Gekul amesisitiza kuwa Serikali Serikali ipo tayari kushirikiana na wanatasnia ya filamu katika kuendeleza Sekta ya filamu nchini ikiwa ni pamoja na kutengeneza mazingira rafiki na wezeshi yatakayo wawezesha wanatasnia wa ndani na nje ya nchi kufanya shughuli zao nchini.

Aidha, amesema yapo maeneo  kadhaa muhimu ambayo Tanzania inaweza kushirikiana na Marekani katika filamu na ikanufaika nayo.


Ameyataja maeneo hayo  kuwa ni pamoja  na utayarishaji wa filamu kwa kutumia mandhari zinazo patikana katika nchi zote mbili, Usambazaji (Uuzaji) wa filamu za ndani ambapo amefafanua  kuwa ipo haja ya kusambaza filamu zinazozalishwa hapa nchini kwa hadhira kubwa zaidi ikizingatiwa kwamba  Tanzania inazalisha takriban filamu 1400 kila mwaka ambazo hurekodiwa kwa lugha ya Kiswahili ambayo inazungumzwa na takribani watu milioni 150 duniani. 

Maeneo mengine ni kuwa  na eneo Changamani la Filamu na  kuandaa matamasha na Tuzo za Filamu za Kimataifa kama vile Tamasha la Filamu la Lake International Pan African la Kenya, Tuzo ya OUMAROU Ganda Price ya Bukina Faso, Tuzo za Hollywood na African Prestigious Awards (HAPAWARDS) za Marekani, Tuzo za World Oscar Signature za Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Tuzo za African Magic Viewer’s Choice Awards (AMVCA) za Nigeria, na Tuzo za ZIMOKO  za  Zambia.

Mbali  na wadau mbalimbali kuhudhuria semina hiyo pia Mwenyekiti wa Kamati ya Filamu ya Royal Tour ambaye  pia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo. Dkt, Hassan Abbasi amehudhuria ambapo Mhe. Gekul amempongeza kwa kazi nzuri aliyoifanya.

Naye, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Abbasi amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mhe,  Samia suluhu Hassan amefanya kazi kubwa  ya kuiandaa  na kwamba  watanzania wanapaswa kumpongeza   kwa ujasiri na kuwa mstari wa mbele kufanikisha filamu hii.


 

Post a Comment

Previous Post Next Post