SERIKALI YATOA TAHADHARI YAKUWAFUNGIA LESENI WAFANYABIASHARA WANAOPANDISHA BEI ZA MBOLEA KIHOLELA






 Baadhi ya wafanyabiashara ambao wameshiriki kwenye kikao hicho.

……………………….

NA MUSSA KHALID

Serikali imewataka wafanyabiashara wa Mbolea Nchini kutumia vizuri uhuru wa soko uliotolewa na Waziri bila ya kuwaumiza wakulima kwa kupandisha bei kiholela.

Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dar es salam na Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti Mbolea Nchini- TFRA Dkt Stephan Ngailo wakati akizungumza na wafanyabiashara wa Mbolea kutoka katika makampuni mbalimbali ambapo amesema serikali itakuwa tayari kuwafungia leseni wafanyabiashara wote watakaokiuka maelekezo hayo.

Dkt Ngailo amesema siku za hivi karibuni kumekuwa na utaratibu wa kupandisha bei za Mbolea mara kwa mara kwa baadhi ya wauzaji /wasambazaji bila kuwepo sababu hivyo kusababisha usumbufu Kwa wakulima.

Amesema kwa mujibu wa tathmini ambayo wameifanya mwezi Februari na mwezi Machi mwaka huu kumekuwa na mabadiliko ya ongezeko la bei linalozidi zaidi ya asilimia 40 mpaka 50 katika eneo moja kwa bei ya aina moja na hivyo kusababisha changamoto kwa wakulima hasa katika mikoa ya Nyanda za juu kusini.

“Kwa mfano bei ya Mbolea ya Urea kwa mfuko wa kilo 50 Kwa mwezi Machi,2022 Mkoa wa Njombe bei 145,000-150,000,Ruvuma Tsh 130,000 na Katavi Tsh 145,000″amesema Dkt Ngailo

Aidha amesema kutokana na tathmini ya awali ilivyoonesha,serikali inaangalia uwezekano wa kurejesha utaratibu wa kuwa na bei elekezi Kwa Mbolea zote kuu ukiwemo Urea,DAP,CAN,na SA.

“Maelekezo ya serikali  kwa wafanyabiashara wakati wa kuruhusu soko huria na kuondoa bei elekezi ilikuwa ni kutokutumia vibaya uhuru huo kwa kupandisha bei kiholela hivyo kimsingi hatutasita kumfutia leseni mfanyabiashara ambaye atapandisha bei hizo hizo’amesema Dkt Ngailo

Dk Ngailo amesema TFRA itaendelea kushirikiana na wadau wote kuhakikisha wakulima wote wa Tanzania wanapata Mbolea Kwa wakati na kwa bei halisia ya soko la dunia na ndani.

Hata hivyo amewataka wafanyabiashara kuhakikisha wanafanya biashara kwa kuzingatia sheria ya Mbolea namba 9 ya mwaka 2009 sambamba na kufata kanuni zake zilivyo na kubadili utaratibu wa bei yawe ni shirikishi na sio kujipangia.

Post a Comment

Previous Post Next Post