TBS,TAASISI YA NELSON MANDELA WAINGIA MAKUBALIANO YA UPIMAJI FILTER ZA MAGARI

 Afisa Viwango TBS, Bw.Arnold Mato (katikati) akizungumza na waandishi wa habari leo katika ofisi za makao makuu ya TBS Jijini Dar es Salaam. Afisa Sheria wa TBS, Lucy Mallya akizungumza na waandishi wa habari leo katika ofisi za makao makuu ya TBS Jijini Dar es Salaam.

**************************

NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) wameingia kwenye Hati Makubaliano na Taasisi ya elimu ya juu ya chuo cha Sayansi na Teknolojia cha Nelson Mandela kwa lengo la kupima filter za magari.

Taasisi hiyo ambayo imeingia kwenye hati ya Makubaliano na TBS, itakuwa na jukumu la kupima filter za kwenye magari zinazotengenezwa hapa nchini na zinazoingia kutoka nje ya nchi.

Akizungumza na Waandishi wa Habari leo Tarehe 22/03/2022 Jijini Dar es Salaam, Afisa Viwango TBS, Bw.Arnold Mato amesema wameingia makubaliano na Taasisi hiyo kutokana na taasisi hiyo kuwa na maabara zenye umahiri na uwezo wa kupima filter za kwenye magari.

Amesema wameandaa viwango vya upimaji wa filter za aina mbili, kuna kiwango cha TZS 2308 ikiwa ni filter za kuchuja hewa ya AC, kiwango cha TZS 1956 kiwango cha filter zinazochuja hewa inayoingia kwenye injini.

Aidha amesema TBS wanaviwango vya Kitanzania vya aina mbili ambavyo ni viwango vya lazima na viwango visivyo vya lazima, viwango vya filter za kwenye magari ni viwango vya lazima kwasababu vinahusiana moja kwa moja kwenye afya na uchumi.

Bw.Arnold amesema kuna umuhimu mkubwa kwa watumiaji wa magari kuhakikisha wanabadilisha filter mara tu zitakapoisha muda wake pale ambapo ataweza kuambiwa na fundi kuna ulazima wa kubadilisha kwasababu kazi kubwa ya filter ni kuchuja hewa inayoingia kwenye injini au kwenye AC na kuweza kumlinda mtumiaji.

“Tumeandaa viwango hivi kutokana natafiti zilizotoka sehemu mbalimbali kama kwenye taasisi za elimu ya juu zikionesha kwamba kuna umuhimu wa kujihakikishia kwamba filter zinazozalishwa nchini na zinazoagizwa nje zinakaguliwa na zinahakikiwa ubora wake kwa kuwa zina madhara moja kwa moja ya usalama pamoja uchumi”. Amesema Bw.Arnold.

Kwa upande wake Afisa Sheria wa TBS, Lucy Mallya amewaasa wafanyabiashara wote wanaojihusisha na filter za magari wawasilishe bidhaa zao TBS ili ziweze kupimwa na kuhakikiwa ubora dhidi ya Viwango husika.

Amesema kifungu cha 20(6) cha Sheria ya Viwango Sura ya 130 kinamkataza mtu yeyote kuuza,kutengeneza, kusambaza au kuchakata bidhaa yoyote ambayo inakwenda kinyume na matakwa ya kiwango husika kilichotangazwa na Waziri mwenye dhamana ya Masuala ya Uwekezaji,Viwanda na Biashara.

Hata hivyo ameelezea adhabu iliyoainishwa chini ya Kifungu cha 27 cha Sheria ya Viwango kwa mtu yeyote atakaye kiuka kifungu chochote kilichotungwa chini ya Sheria ya Viwango.Kwa mujibu wa kifungu hicho cha 27,mtu yeyote atakayethibitika kukiuka masharti ya kifungu chochote cha Sheria ya Viwango atapewa adhabu ya kifungo kisichopungua miaka miwili au faini ya shilingi milioni hamsini hadi mia moja au adhabu zote mbili kwa pamoja.

Post a Comment

Previous Post Next Post