Maafisa Utamaduni na Michezo nchi nzima kupewa mafunzo ya kusaka vipaji mtaa kwa mtaa- Mhe. Mchengerwa

Na. John Mapepele

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe, Mohamed Mchengerwa amesema Wizara imeandaa kikao kazi cha Maafisa Utamaduni na Michezo  wote nchi nzima ili kuwapa mafunzo maalum ya kusimamia na kutekeleza  mpango wa kitaifa wa kuibua vipaji utakaoanzisha  ligi kuanzia  kwenye  ngazi ya Kijiji na mtaa  hadi taifa  ili kupata timu bora za taifa  katika michezo mbalimbali.

Mhe. Mchengerwa amesema hayo leo Machi 22, 2022 alipokuwa akifungua semina kwa Kamati ya  Kudumu ya Bunge  ya  Huduma  na Maendeleo ya Jamii katika ukumbi wa Bunge jijini Dodoma  na amesema kikao hicho kitafanyika Aprili 5-6, 2022 mjini Dodoma na kinatarajiwa  kufunguliwa na Waziri Mkuu Mhe, Kassim Majaliwa.

Amefafanua kuwa ligi hii ni mpango maalum wa Serikali wa kuendeleza michezo ambao unatekeleza dhana ya kuibua wachezaji kuanzia chini ya mtaa kwa mtaa. 

Mbali na kuanzisha ligi hizo Mhe. Mchengerwa ametaja mambo mengine makubwa ambayo wizara  yake  inakwenda  kuyafanya mwezi Aprili kuwa ni pamoja na Wizara inakwenda kuzindua Mpango Mkakati wa michezo ambao utaainisha kazi gani inafanywa lini na nani ili kuboresha michezo. 

Aidha, amesema Wizara  inakwenda  kujenga  miundombinu ya kisasa kwenye  shule za Sekondari za wavulana na wasichana za  Tabora  mkoani Tabora ambazo zitatumika kwenye mashindano ya Umiseta na Umitashumta  ya mwaka huu.

Kwa upande mwingine amesema tayari Serikali imeshajenga viwanja changamani vya michezo vinne ambapo viwili kwa kanda ya Pwani mkoa wa Dar es Salaam na viwili mkoani Tanga ambapo miundo yote imeshafika zaidi ya asilimia 80.

Kuhusu ujenzi wa kiwanja cha kisasa jijini Dodoma, Mhe. Mchengerwa amesema Serikali itahakikisha ujenzi huo unakamilika kabla ya 2025 ambapo amefafanua kuwa hadi sasa michoro imekamilika na tayari wadau kadhaa wamejitokeza kuwekeza.

Mwenyekiti Kamati hiyo Stanslaus Nyongo amemshukuru na kumpongeza Mhe. Waziri kwa ubunifu mkubwa ambapo amesema anaimani kuwa anakwenda  kuleta mapinduzi makubwa ambapo ameishauri Wizara  kushirikisha wadau wa sekta binafsi kwenye  kuwekeza kwenye michezo.

Aidha, ameiomba Wizara  kuijengea  uwezo  Kamati ili iweze kuiomba Serikali kutoa punguzo zaidi  kwenye vifaa vya  michezo.

Mbunge wa viti maalum na  Mjumbe wa Kamati hiyo, Neema Lugangira amepongeza ubunifu wa Wizara wa kuanzisha   ligi ya mtaa kwa mtaa ambapo pia amewashauri wajumbe wote wa Kamati  kuiomba Serikali kutoa gharama za kupima Uviko na MRI.

Katika semina hiyo Wizara iliwapitisha wajumbe katika mada ya kufanya vizuri katika michezo iliyowasilishwa na Kaimu Katibu wa Baraza la Michezo (BMT) bi Neema Msitha na Mada ya taarifa ya mafanikio ya Shirikisho la Soka nchini (TFF) Alfred Kidau.






Post a Comment

Previous Post Next Post