Jane Edward, Arusha
Tume ya Taifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu (COSTECH)imetakiwa kuendelea kuunga mkono watafiti mbalimbali hapa nchini ikiwemo tafiti za mazao mchanganyiko ili kuendelea kuzalisha vijana wabunifu zaidi.
Akizungumza na Michuzi Blog Mkurugenzi wa kampuni ya Imara teknoloji Alfred Chengula inayojihusisha na shughuli za uzalishaji wa mashine za kilimo jijini Arusha
Amesema Costech imekuwa kimbilio la watafiti wengi katika kuendeleza teknolojia hapa nchini hali inayofanya vijana wengi kuendelea kufanya tafiti na kubuni mashine mbalimbali zenye tija.
Kupitia msaada wa Costech Imara Tech imeweza kubuni mashine yenye uwezo wa kupura na kupeta mazao aina tisa (9) tofauti kwa ajili ya wakulima wadogo wadogo ambayo imepata umaarufu mkubwa sana na kuweza kuwafikia zaidi ya wakulima mia nne (400) na kuuzwa Nchi za nje kama vile; Zambia, Malawi, Rwanda, Burundi, Kenya, Uganda, Zimbabwe na Malawi.
Amefafanua kuwa mashine hizo zimesaidia kuajiri vijana zaidi ya 290 ambapo hutumia mashine hizo kwa ajili ya kujiingizia kipato na kupunguza nguvu kazi kubwa ambayo utumiwa na wakulima kipindi cha uvunaji.
Alfred ameeleza kuwa pamoja na mafanikio hayo, kampuni ya Imara inaendelea kufanya utafiti kwa zana nyingine ambazo zinaweza kuongeza tija kwenye jamii na kwa sasa wapo kwenye utafiti ambapo wamebuni mashine tatu tofauti ambazo ni mashine ya kukamua mafuta ya parachichi kwa kushirikiana na kampuni ya Avomeru, Mashine ya kumenya karanga pamoja na mashine ya kusaga.
"Mashine hizo zote zipo kwenye hatua ya majaribio na pindi zikikamilika basi zitaenda kuongeza tija kwa watumiaji" Alisema Alfred
Ameongeza kuwa kwa sasa wamepata ufadhili wa mashine ya kisasa ya kukata chuma kwa kutumia kompyuta (Laser Cutter) japo mashine hiyo haijaanza kutumika na kama ikianza kutumika basi itaenda kuongeza uzalishaji kwa kiasi kikubwa na kuongeza ajira kwa Watanzania hivyo ameomba msaada kwa Costech kuendelea kutoa ushirikiano ili kuahakikisha mazingira ya uzajilishaji yanakuwa rafiki.
Hata hivyo hivi karibuni Serikali kupitia Costech iliwakutanisha waandishi wa habari na watafiti kwa lengo la kubadilishana uzoefu hasa katika masuala ya Sayansi na Costech kuahidi ushirikiano kwa watafiti na waandishi hao.
Mkurugenzi wa Imara Teknoloji Alfred Chengula akielezea kuhusiana na mashine waliyoitafiti kwa Kaimu Mkurugenzi wa COSTEC Philbert Luhunga.
Mkulima akijaribu kupukuchua mahindi kwenye mashine ya Imara teknoloji.
Wakulima wakiangalia mifugo ikifurahia pumba iliyopukuchuliwa na mashine iliyopo pichani.