Waziri Mchengerwa atoa maelekezo mazito ya kuboresha soka nchini

 Na. John Mapepele

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe, Mohamed Mchengerwa leo Februari 14, 2022 ametoa maelekezo mazito kwa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) na Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) yanayolenga kuboresha mchezo wa mpira wa miguu nchini.

Maelekezo hayo ameyatoa katika mkutano wa Waandishi wa Habari aliofanya katika Ukumbi wa Uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam leo Februari 14 baada ya kufanya kikao na Viongozi wa TFF, BMT na watendaji wa Wizara.

Amefafanua kuwa Serikali ipo katika mikakati kabambe ya kuboresha miundombinu ya michezo katika shule 56 nchini ikiwa ni pamoja na kufunga mashine za kisasa za kufuatilia michezo (VAR) kwenye  viwanja vitano  kwa kuanzia pamoja na kujenga  vituo  vikubwa vya michezo.

Akitoa  maelekezo ya Serikali,  Mhe. Mchengerwa amesema BMT likutane na TFF mara moja kujadili namna ya  kudhibiti vitendo  vya  ukiukwaji wa Sheria na taratibu za mchezo huo pendwa nchini ambapo pia amesisitiza  kuwa Kamati inayohusika na Waamuzi ijitafakari kwa kuwa hadi sasa kwenye msimu huu wa ligi tayari imeshawaondoa waamuzi 13 kwa makosa ya upendeleo na rushwa.

Pia amesema TFF likutane na waamuzi wote ili kupata uvumbuzi wa changamoto na sintofahamu zinazoendelea kujitokeza katika mchezo huo kinyume na sheria ambapo TAKUKURU washirikishwe wawepo ili waweze  kutoa elimu ya rushwa  kwenye mchezo wa mpira wa miguu.

Amefafanua kuwa iwapo Serikali  haitaweza kudhibiti vitendo vya rushwa kwenye mchezo wa mpira wa miguu, mchezo huo  hautakuwa na maendeleo.

Aidha, amesisitiza waamuzi wasio na sifa waondolewe moja kwa moja  na kuwaleta wengine  wenye sifa na   TFF lihakikishe utekelezaji wa sheria na kanuni za vilabu huku BMT iendelee kusimamia  utawala bora ili kuwe  na ustawi  katika michezo.

Pia ameviomba Vyombo vya Habari kuelimisha jamii  kuhusu programu mbalimbali za redio na televisheni kuhusu sheria za mpira wa miguu kupitia kwa wakufunzi na waamuzi.

Katika  mkutano huo Mhe. Mchengerwa aliambatana na Katibu Mkuu wa Wizara yake Dkt. Hassan Abbasi, na Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya michezo na Kaimu katibu Mtendaji wa Baraza la Michezo la Taifa(BMT) na   Uongozi wa TFF






Post a Comment

Previous Post Next Post