Na. John Mapepele
Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo amekitaka chama cha kuogelea nchini kushirikisha mikoa yote nchini ili kupata waogeleaji wenye vipaji watakaoiwakilisha vema Tanzania kwenye mashindano ya kimataifa.
Mhe. Gekul ameyasema haya leo Disemba 4, 2021jijini Dar es Salaam allipoambatana na Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza la Michezo la Taifa( BMT) Neema Msitha kuikabidhi bendera na kuiaga timu ya Tanzania inayokwenda kushiriki mashindano ya Afrika ya kuogelea nchini Uganda.
Aidha, amewapongeza wazazi kwa kuwaruhusu watoto kushiriki katika mchezo huu.
"Niwapongeze wazazi kwa mwamko mkubwa wa kuwarushusu watoto kujiunga kwenye mchezo huu, hii itasaidia kupata vipawa na vipaji vingi " amefafanua Mhe. Gekul
Amesema Serikali imeshaandaa Mpango Mkakati wa miaka kumi wa kuinua na kuendeleza michezo ili kuinua michezo.
Naye Msitha amemweleza Mhe. Naibu Waziri kuwa chama cha mchezo wa kuogelea ni miongoni mwa vyama vya michezo inayofanya kazi nzuri ya kuinua mchezo huu hapa nchini.
Kiongozi wa timu hiyo Inviolata Itatilo amesema nchi zaidi ya kumi za Afrika zinashiriki mashindano haya nchini Uganda.