WAZIRI JAFO AWEKA WAZI MAFANIKIO YA OFISI YA MAKAMU WA RAIS MUUNGANO NA MAZINGIRA TANGU UHURU

 

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Selemani Jafo,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo November 15,2021 jijini Dodoma wakati akitoa taarifa kuhusu mafanikio ya sekta ya Muungano na Mazingira katika kipindi cha miaka 60, ya Uhuru wa Tanganyika.

Baadhi ya waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali wakifatilia hotuba ya Waziri  wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Selemani Jafo (hayupo pichani) wakati akitoa taarifa kuhusu mafanikio ya sekta ya Muungano na Mazingira katika kipindi cha miaka 60, ya Uhuru wa Tanganyika leo November 15,2021 jijini Dodoma

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Selemani Jafo,akijibu maswali ya waandishi wa habari (hawapo pichani) leo November 15,2021 jijini Dodoma mara baada ya kutoa  taarifa kuhusu mafanikio ya sekta ya Muungano na Mazingira katika kipindi cha miaka 60, ya Uhuru wa Tanganyika.

………………………………………………………

Na.Alex Sonna,Dodoma

WAZIRI wa Nchi,Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira,Seleman Jafo amesema katika kipindi cha miaka 60 ya uhuru wa Tanzania Bara ni kuanzishwa kwa utaratibu wa kushughulikia hoja za Muungano kupitia vikao vya Kamati ya Pamoja ya SMT na SMZ mwaka 2006 ambapo hoja 25 zimejadiliwa na mpaka sasa hoja 18 zimepatiwa ufumbuzi.

Hayo ameyasema leo November 15,2021 jijini Dodoma wakati akitoa  taarifa kuhusu mafanikio ya sekta ya Muungano na Mazingira katika kipindi cha miaka 60, ya Uhuru wa Tanganyika.

,Waziri Jafo amesema tangu kuanzishwa kwa utaratibu wa kushughulikia hoja za Muungano kupitia vikao vya Kamati ya Pamoja ya SMT na SMZ mwaka 2006 hoja 25 zimejadiliwa na mpaka sasa hoja 18 zimepatiwa ufumbuzi.

Amesema hoja zilizopatiwa ufumbuzi na kuondolewa kwenye orodha ya hoja za Muungano ni pamoja na Utekelezaji wa Sheria ya Haki za Binadamu Zanzibar, Utekelezaji wa Sheria ya Usafirishaji Majini (Merchant Shipping Act) katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Uwezo wa Zanzibar Kujiunga na Shirika la Bahari Duniani (International Maritime Organisation – IMO).

Amezitaja hoja nyingine ni Ushiriki wa Zanzibar katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, Utafutaji na Uchimbaji wa Mafuta na Gesi Asili, Ushiriki wa SMZ katika masuala mbalimbali ya Kimataifa na Kikanda, Gharama za Kushusha Mizigo (Landing Fees) Bandari ya Dar es Salaam kwa Mizigo inayotoka Zanzibar.

Hoja zingine ni  Usimamizi wa Ukokotoaji na Ukusanyaji wa Kodi kwenye Huduma za Simu unaofanywa na Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRB) na Mikataba ya Mikopo ya Fedha za ujenzi wa miradi ya SMZ.

Pia, hoja za Uvuvi katika Ukanda wa Uchumi wa Bahari Kuu, Ajira kwa Watumishi wa Zanzibar katika Taasisi za Muungano, Mgawanyo wa mapato yatokanayo na: Misamaha ya Mikopo ya Fedha kutoka IMF, misaada ya kibajeti (General Budget Support – GBS), na Uwezo wa Zanzibar kukopa ndani na nje ya Nchi zimepatiwa ufumbuzi.

“Kwa kutambua na kuzingatia fursa na changamoto zilizopo, katika miaka ijayo, Serikali inatarajia kwamba Muungano utaimarika na mafanikio yaliyopatikana yataendelezwa kwa lengo la kuinua hali za maisha na ustawi wa wananchi wa pande mbili za Muungano.

“Kuimarika na kudumu kwa Muungano kutakuwa ni nguzo muhimu ya kuendeleza udugu na matarajio ya Waasisi wa Muungano ya kuwa na Tanzania yenye uchumi imara, Amani, utulivu, haki na usawa kwa kila Mtanzania,”amesema.

MITI MILIONI MIA SITA YAPANDWA  

Waziri Jafo amesema Wizara yake imeendelea kuratibu utekelezaji wa Kampeni ya Upandaji miti kwa lengo la kurejesha Uoto wa Asili na kupunguza hali ya kuenea kwa jangwa na ukame ambapo kila Halmashauri ya Wilaya imeelekezwa kupanda miti milioni 1.5 kila mwaka.

Amesema hadi kufikia Mei 2020 takribani miti 608,494,464 ilipandwa katika mikoa yote 26 katika Halmashauri zote. Baada ya tathmini asilimia 62.8 ya miti iliyopandwa ndiyo iliyopona.

“Pamoja na hayo kutokana na umuhimu wa kulinda hifadhi ya bahari, wananchi wameshirikishwa kupanda na kuhifadhi mikoko katika maeneo mbalimbali ya Pwani Tanzania Bara na Tanzania Visiwani hatua inayosaidia kupunguza changamoto ya mabadiliko ya tabianchi,”amesema.

Amesema katika kuhamasisha ushiriki wa jamii kwenye eneo la hifadhi na usimamizi wa mazingira, Ofisi ya Makamu wa Rais imeendelea kuratibu Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani ambayo huadhimishwa kila ifikapo tarehe 5 Juni.

MIKAKATI YA UHIFADHI NA USIMAMIZI WA MAZINGIRA

Waziri Jafo amesema katika kuimarisha hifadhi na usimamizi wa mazingira nchini Mikakati mbalimbali imeandaliwa na kutekelezwa. Mikakati hiyo nipamoja na:

Ametaja mikakati hiyo ni pamoja na Mkakati wa Taifa wa Usimamizi wa Kemikali na Taka Hatarishi wa mwaka (2020 – 2025); Mkakati na Mpango Kazi wa Taifa wa kukabiliana na  Viumbe Vamizi  wa mwaka (2019 – 2029); Mpango- Kazi wa Taifa wa Kupunguza Matumizi ya Zebaki kwa Wachimbaji wadogo wa Dhahabu (2020 -2025);

Ameitaja mikakati mingine ni  Mpango Kazi wa Taifa wa Hifadhi ya Bioanuai (2015 – 2020);  Mkakati na Mpango Kazi wa Taifa kudhibiti kuenea kwa Viumbe Vamizi (2019- 2029) na Mkakati na Mpango Kazi wa Taifa wa kuongoa Mfumo ikolijia ya mto Ruaha (2017-2022).

CHANGAMOTO

Jafo amesema baadhi ya mila na desturi bado zinarudisha nyuma juhudi za kuhifadhi mazingira.

Ametolea mfano, tatizo la uchomaji moto bado ni sugu katika maeneo mengi nchini na moja wapo ya sababu ni mila potofu, mfano; mtu akianzisha moto na ukawaka kwa muda mferu na kutekeleza eneo kubwa basi ana maisha marefu;

Amesema tatizo la mabadiliko ya tabianchi na athari zake ni changamoto kubwa kwa jumuiya ya kimataifa na nchi.

Ameitaja changamoto nyingine ni kutokuwepo kwa mfumo madhubuti wa utunzaji wa takwimu, taarifa na kumbukumbu za masuala ya mazingira na hivyo kusababisha ucheleweshaji wa maamuzi ya kisera na kimkakati;

“Ufinyu wa bajeti ya Serikali kwa ajili ya utekelezaji wa mikakati na programu zinazoandaliwa umepelekea kuendelea kwa uharibifu wa mazingira nchini.

Pia, amesema hali ya ukame katika baadhi ya mikoa inasababisha kutofikiwa kwa malengo ya idadi ya miti inayotakiwa kupandwa na hivyo kurudisha nyuma juhudi za utunzaji wa mazingira hususan katika mikoa ya Dodoma, Arusha, Manyara na Kilimanjaro

Post a Comment

Previous Post Next Post