WAZIRI MKUU ATEMBELEA MITAMBO YA UZALISHAJI MAJI RUVU JUU NA RUVU CHINI

 WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametoa siku tatu kuanzia leo Jumatatu Novemba 15, 2021 kwa wasimamizi wa Bonde la Mto Ruvu wafuatilie njia zote za kuingiza maji katika mto huo ambazo zimechepushwa ziwe wazi ili maji yaweze kuingia na kupunguza changamoto ya upungufu wa maji.

 

Pia, Mheshimiwa Majaliwa amewaagiza wasimamizi wa mabonde yote nchini wasikae maofisini na badala yake wapite katika maeneo yote wanayoyasimamia na wahakikishe yapo salama. “Tumieni sheria iliyoanzisha mamlaka yenu kuhakikisha mnailinda mito na maziwa.”

 

Mheshimiwa Majaliwa ameiagiza Wizara ya Maji itafute chanzo kingine cha maji kitakachosaidiana na Mto Ruvu ili kuhakikisha maji yanapatikana kwa uhakika katika mikoa ya Pwani na Dar es Salaam.

 

Ametoa maagizo hayo leo Jumatatu Novemba 15, 2021 mara baada ya kutembelea Mitambo ya uzalishaji Maji ya Ruvu Juu na Ruvu Chini ili kukagua hali ya uzalishaji na usambazaji wa maji katika Mkoa wa Dar es Salaam pamoja na Pwani.

 

“Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ametoa maelekezo maalumu katika suala zima la upatikanaji wa huduma ya maji kwa wananchi hadi washio vijijini, Wizara ya Maji hakikisheni mnatafuta vyanzo vingine ili malengo hayo yatimie.” Alisema Mheshimiwa Majaliwa

 

Waziri Mkuu alieleza kuwa Mto Ruvu umeathirika na shughuli za kibinadamu zinazochangia maji kupungua, hivyo wahusika wasimamie ipasavyo ili kupunguza tatizo hilo. Amesema idadi kubwa ya mifugo katika maeneo hayo inaathiri chanzo hicho.

 

Mheshimiwa Majaliwa ameziagiza Wizara za Maji, Maliasili na Utalii, na Mifugo na Uvuvi zikutane na kuona namna bora ya kuboresha mazingira ya ufugaji ili Mto Ruvu ubaki kwa ajili ya kuzalisha maji katika Mikoa ya Pwani na Dar es Salaam.

 

Waziri Mkuu ameiagiza Wizara ya Mifugo na Uvuvi wakazungumze na wafugaji na waweke utaratibu wa kuratibu shughuli za ufugaji bila ya kuathiri chanzo hicho cha maji. “Mifugo tunaihitali lakini lazima iratibiwe.”

 

Amesema elimu ya ufugaji bora lazima itolewe kwa wafugaji, mfano mtu mmoja anapopeleka ng’ombe 1,000 kwenda kuwanywesha maji mtoni wanaathiri watu wengi kwani kitendo hicho kinaathiri vyanzo vya maji na kusababisha upungufu.

 

Naye, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amesema licha ya Serikali kufanya uwekezaji mkubwa katika mitambo ya kuzalishia maji ya Ruvu Chini na Ruvu Juu ili kuhakikisha wakazi wa mikoa ya Dar es Salaam na Pwani wanapata maji ya kutosha. “Vyanzo hivyo vina uwezo wa kuzalisha maji lita milioni 520 huku mahitaji yakiwa ni lita milioni 544.”

 

Amesema kutokana na changamoto ya mabadiliko ya tabianchi kwa sasa vyanzo hivyo vinazalisha lita milioni 350. Amesema ili kukabaliana na changamoto hiyo Wizara inafikiria kuwekeza katika mradi wa Mto Rufiji ambao utasaidia kumaliza tatizo la upatikanaji wa maji katika mikoa hiyo.

 

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) Mhandisi Cyprian Luhemeja amesema kwa sasa hali ya uzalishaji wa maji imepungua kutoka lita milioni 520 hadi lita milioni 460 kwa siku.

Amesema kupungua huko kunatokana na sababu mbalimbali zikiwemo za mabadiliko ya hali ya hewa pamoja na kuwepo kwa makundi makubwa ya mifugo katika eneo la chanzo cha Mto Ruvu.

“Mtambo wa Ruvu Chini ndio ambao umeathirika zaidi kutokana na changamoto ya kupungua kwa kina cha maji katika Mto Ruvu. Kwa sasa, uzalishaji umepungua kutoka lita za ujazo milioni 270 kwa siku hadi lita za ujazo milioni 119.459.” Alisema Mhandisi Luhemeja

Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa akipata maelezo kutoka kwa Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es salaam (DAWASA) Mhandisi Cyprian Luhemeja kuhusu kiwango cha maji cha Ruvu Chini kilivyopungua wakati wa ziara yake ya kutembelea kwenye mitambo ya kuzalishia maji ya Ruvu Chini na Ruvu Juu leo pamoja na kujua sababu kubwa ya mgao wa maji unaendelea katika mkoa wa Dar es Salaam na Pwani.
Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa  akitoa maelekezo kwa uongozi wa DAWASA pamoja na Wizara ya Maji kuangalia namna wanavyoweza kutafuta njia kuweza kutatua changamoto ya mgao wa maji katika maeneo ya Mkoa wa Dar es Salaam na Pwani alipofanya ziara kwenye Mtambo wa kuzalishia maji wa Ruvu Chini na kujionea kupungua kwa kina cha maji cha mto huo.
Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa akipata maelezo kutoka  kwa Katibu Mkuu, Wizara ya Maji Mhandisi Anthony Sanga kuhusu namna wizara hiyo ilivyojipanga kusimamia Mamlaka za maji hasa kwenye Miradi mikubwa ya maji ili kufanikisha upatikanaji wa majisafi na salama kwa wananchi wakati wa ziara yake ya kukagua Mitambo ya Kuzalisha maji ya Ruvu Juu na Ruvu Chini. 
Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa akitoa maelekezo kwa Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es salaam (DAWASA) Mhandisi Cyprian Luhemeja kuhusu Mtambo wa kuzalishia maji wa Ruvu Juu kuhusu namna unavyoweza kusaidia kupunguza uhaba wa maji kwenye mkoa wa Dar es Salaam na Pwani wakati wa ziara yake ya kukagua Mitambo ya Kuzalisha maji ya Ruvu Chini na Ruvu Juu leo.
Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa akipewa maelezo kutoka kwa Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es salaam (DAWASA) Mhandisi Cyprian Luhemeja kuhusu Mtambo wa kuzalishia maji wa Ruvu Juu unavyofanya kazi yake wakati wa ziara yake ya kukagua Mitambo ya Kuzalisha maji ya Ruvu Juu na Ruvu Chini.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es salaam (DAWASA) Mhandisi Cyprian Luhemeja akitoa maelezo kwa Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa, Waziri wa Maji, Jumaa H. Aweso pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge kuhusu namna uzalishaji wa maji wa Ruvu Juu unavyotekelezwa na DAWASA wakati wa Ziara ya Waziri Mkuu ya kukagua Mitambo ya Kuzalisha maji ya Ruvu Juu na Ruvu Chini leo
Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa akizugumza na viongozi wa Wizara ya Maji, DAWASA pamoja na waandishi wa habari kuhusu namna alivyotembelea Mtambo wa kuzalishia maji wa Ruvu Juu na Ruvu Chini na kujionea changamoto wanazozipitia Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es salaam (DAWASA)  mara baada ya kitangaza mgao wa maji katika mkoa wa Dar es Salaam na Pwani.
Waziri wa Maji, Jumaa H. Aweso akizungumza na wafanyakazi wa Wizara ya Maji, wafanyakazi wa DAWASA pamoja na waandishi wa habari kuhusu namna walivyojipanga kama Wizara ili kuweza kuwapatia wananchi majisafi na salama mara baada ya kumalizika kwa Ziara ya Waziri Mkuu ya kukagua Mitambo ya Kuzalisha maji ya Ruvu Juu na Ruvu Chini leo. Wa kwanza kushoto ni Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa na katikati ni Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es salaam (DAWASA) Mhandisi Cyprian Luhemeja

Post a Comment

Previous Post Next Post