Matuko katika Picha wakati wa uzinduzi wa Ligi ya Taifa ya Mpira Wa Kikapu iliyopewa jina la “CRDB BANK TAIFA CUP,” katika viwanja vya Chinangali jijini Dodoma.
*************************
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Innocent Bashungwa amesema Serikali kupitia Wizara yake tayari imetangaza zabuni ya kimataifa, ya usanifu wa viwanja viwili vya kisasa mahususi kwa ajili ya michezo ya ndani (sports and arts arena), katika jiji la Dar es Salaam na Dodoma.
Waziri Bashungwa ametoa kauli hiyo leo Novemba 5, 2021, wakati akizindua Ligi ya Taifa ya Mpira Wa Kikapu iliyopewa jina la “CRDB BANK TAIFA CUP,” katika viwanja vya Chinangali jijini Dodoma.
Amesema ili kuendelea kuimarisha michezo hususani michezo ya ndani (indoor games), Serikali inaendelea na mikakati ya kuhakikisha inajenga viwanja hivyo viwili kama sehemu ya uboreshaji wa miundo mbinu ya michezo hapa nchini.
Kwa Mujibu wa Waziri Bashungwa Mchezo wa kikapu ni moja kati ya michezo sita (6) iliyopewa kipaumbele na Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa imani kuwa, ukifanyika uwekezaji wa kutosha mchezo huo unaweza kutoa fursa kwa vijana wengi wa kitanzania.
Awali akizungumza katika uzinduzi huo Rais wa Chama cha Mpira wa Kikapu Tanzania Phares Magesa amesema Chama hicho kinaendelea na jitihada mbalimbali katika kuhakikisha Mpira wa Kikapu unaendelea kukonga nyoyo za watazamaji huku akihaidi kuwa watahakikisha wanaufanya mchezo huo kuwa miongoni mwa michezo pendwa hapa nchini.
Kwa upande wake afisa uendeshaji Mkuu wa Benki ya CRDB ambayo ni mdhamini mkuu wa ligi hiyo bwana Bruce Mwile, amepongeza hatua ya Serikali ya kukusanya asilimia tano kutoka kwenye michezo ya kubahatisha itakayopelekwa kwenye mfuko wa maendeleo ya michezo akisema kiasi hicho kinachokusanywa na serikali kwa ajili ya kutunisha mfuko huo kitasaidia kuinua michezo iliyopewa kisogo na watu wengi kwa sabau ya ukata kwenye michezo husika.