WIZARA YA MAJI KUNUNUA VIFAA VYA KISASA KWA AJILI YA KUFANYA UTAFITI WA MAJI ARDHINI

 

WAZIRI wa Maji Mhe.Jumaa Aweso ,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani)  leo Oktoba 27,2021 jijini Dodoma wakati akitoa taarifa kuhusu matumizi ya fedha za Mgao wa kutekeleza miradi katika athari za uviko -19.

Baadhi ya Watendaji wa Wizara ya Maji wakifatilia hotuba ya Waziri wa Maji Mhe.Jumaa Aweso (hayupo pichani)  wakati akitoa taarifa kuhusu matumizi ya fedha za Mgao wa kutekeleza miradi katika athari za uviko -19  leo Oktoba 27,2021 jijini Dodoma

Katibu Mkuu Wizara ya Maji Mhandisi Anthony Sanga ,akizungumza kabla ya kuingia Mkataba na Kampuni ya CRJE East Afrika Limited kwa ajili ya ujenzi wa jengo la Wizara hiyo ujenzi utakaogharimu kiasi cha shilingi bilioni 22.9 hadi utakapo kamilika

Katibu Mkuu Wizara ya Maji Mhandisi Anthony Sanga akisaini  Mkataba na Kampuni ya CRJE East Afrika Limited kwa ajili ya ujenzi wa jengo la Wizara hiyo Mtumba ujenzi utakaogharimu kiasi cha shilingi bilioni 22.9 hadi utakapo kamilika.

Katibu Mkuu Wizara ya Maji Mhandisi Anthony Sanga akibadilishana Mkataba mara baada ya kuingia na Kampuni ya CRJE East Afrika Limited kwa ajili ya ujenzi wa jengo la Wizara hiyo Mtumba ujenzi utakaogharimu kiasi cha shilingi bilioni 22.9 hadi utakapo kamilika.

………………………………………………………….

Na.Alex Sonna,Dodoma

WAZIRI wa Maji Mhe.Juma Aweso amesema kupitia fedha za mradi wa mapambano dhidi ya athari za uviko -19 Wizara hiyo imepanga kununua seti nne za vifaa vya kisasa kwa ajili ya kufanya utafiti wa maji ardhini ili kuondoa kadhia ya awali ya kutumia fedha nyingi kuchimba visima katika maeneo mbalimbali bila kuwa na uhakika wa kupata maji.

Kauli hiyo ameitoa leo Oktoba 27,2021 jijini Dodoma  wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu matumizi ya fedha za Mgao wa kutekeleza miradi katika athari za uviko -19, ambapo Wizara hiyo imepata kiasi cha shilingi bilioni 139.4 ambapo kiasi kati ya fedha hizo zitatumika kununua vifaa hivyo vya kufanya utafiti wa maji ardhini na kutekeleza miradi 218 nchi nzima.

Aweso amesema wizara imeeelekeza  Sh 17,613,853,330 kwa ajili kununua sekta tano za mitambo ya ujenzi wa mabwawa  na seti nne za vifaa vya kisasa vya utafiti wa maji chini ya ardhi.

” Kwa muda mrefu Serikali na wadau wameekuwa wakichimba visima maeneo mbalimbali nchini bila kuwa na uhakika wa kupata maji  kwa kutambua umuhimu wa utafiti maji chini ya ardhi kabla ya kuanza kuchimbia tunanunua vifaa vya kisasa vya utafiti.”amesema Aweso

Aidha Aweso amesema kuwa  wamepanga  kununua seti 25 ya mitambo ya kuchimbia visima ambavyo kila mkoa utapata mtambo mmoja, lengo likiwa ni kukabiliana na uhaba wa vitendea kazi na kusisitiza kuwa Wizara itahakikisha mitambo hiyo inatunzwa.

” Tumekuwa na uhaba wa vitendea kazi hususani mitambo ya kuchimbia visima ambapo husababisha kuchelewesha utekelezaji wa miradi na hatimaye upatikanaji wa huduma za maji kwa wananchi.”amesema Aweso

Katika hatua nyingine Mhe. Aweso ameagiza watendaji wote watakao simamia miradi hiyo kusimamia kwa weledi na Wizara itafuatilia kwa ukaribu sana utekelezaji wa miradi hiyo.

” Mimi na viongozi wengine wa wizara tutafuatilia kwa karibu utekelezaji wa Mpango huu na kwa yeyote ambaye atakwamisha malengo hatutavumilia na tutachukua hatua kali”amesisitiza

Wakati huo huo Wizara ya Maji imesaini mkataba na Kampuni ya CRJE East Afrika Limited wa ujenzi wa jengo la Wizara hiyo ujenzi utakaogharimu kiasi cha shilingi bilioni 22.9 hadi utakapo kamilika.

Katibu Mkuu Wizara ya Maji Mhandisi Anthony Sanga ameitaka Kampuni hiyo kuzingatia ubora katika utekelezaji wa mradi huo.

Post a Comment

Previous Post Next Post