WAZIRI MAKAMBA AKUTANA NA MAKAMU WA RAIS EQUINOR – AFRICA

 

Makamu wa Rais wa Equinor (Afrika) Bw. Paul McCafferty akimweleza jambo Waziri wa Nishati Mh. January Yusuf Makamba wakati wa kikao kifupi kilichofanyika Oktoba 21, 2021 katika ofisi ndogo za Wizara ya Nishati jijini Dar es Salaam. Pamoja nao, ni viongozi wengine wa Equinor na Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini (TPDC) waliohudhuria kikao hicho.

Waziri wa Nishati Mh. January Yusuf Makamba akimsikiliza  Makamu wa Rais wa Equinor (Afrika) Bw. Paul McCafferty wakati wa kikao kifupi kilichofanyika Oktoba 21, 2021 katika ofisi ndogo za Wizara ya Nishati jijini Dar es Salaam. Pamoja nao, ni viongozi wengine wa Equinor na Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini (TPDC) waliohudhuria kikao hicho.

Waziri wa Nishati Mh. January Yusuf Makamba akizungumza jambo na Makamu wa Rais wa Equinor (Afrika) Bw. Paul McCafferty wakati wa kikao kifupi kilichofanyika Oktoba 21, 2021 katika ofisi ndogo za Wizara ya Nishati jijini Dar es Salaam. Pamoja nao, ni Makamu wa Rais na Mwenyekiti Mkazi, Equinor Tanzania AS, Unni Merethe Skolstad Fjaer (katikati) na Mkuu wa Idara ya Mawasiliano Equinor Tanzania, Genevieve Kasanga.

Waziri wa Nishati Mh. January Yusuf Makamba, (Wa pili kutoka kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Makamu wa Rais wa Equinor (Afrika) Bw. Paul McCafferty, Makamu wa Rais na Mwenyekiti Mkazi, Equinor Tanzania AS, Unni Merethe Skolstad Fjaer (kulia kwa Waziri Makamba) na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC) Dkt. James Mataragio, mara baada ya kikao kifupi kilichofanyika Oktoba 21, 2021 katika ofisi ndogo za Wizara ya Nishati jijini Dar es Salaam.

………………………………………………………………….

Na Janeth Mesomapya

Waziri wa Nishati Mh. January Yusuf Makamba amekutana na kufanya mazungumzo na Makamu wa Rais wa kampuni ya utafutaji na uzalishaji wa mafuta na gesi asilia ya Equinor (Afrika) Bw. Paul McCafferty.

Viongozi hao wamekutana Oktoba 21, 2021 katika ofisi ndogo za Wizara ya Nishati zilizopo jijini Dar es Salaam. Mazungumzo hayo yamehudhuriwa pia na viongozi wengine wa Equinor na Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini (TPDC).

Imeelezwa kuwa mazungumzo hayo ni sehemu ya maandalizi ya majadiliano ya Mkataba wa Nchi Hodhi (HGA) wa Mradi wa Kuchakata na Kusindika Gesi Asilia (LNG) yanayotarajiwa kuanza rasmi Novemba 8, 2021.

Kwenye kikao hicho, Bw. McCafferty amempongeza Waziri Makamba kwa niaba ya serikali kwa hatua hiyo ya kuanza tena kwa majadiliano ya mkataba huo wa HGA kwani yatafungua njia kwaajili ya kuanza kwa utekelezaji wa mradi huo wa LNG.

Bw. McCafferty ameeleza kuwa Equinor iko tayari kwa majadiliano hayo na kuongeza kwamba mradi huo ni moja ya miradi yenye uwekezaji mkubwa inayotekelezwa na Equinor duniani, hivyo ni majadiliano muhimu katika kuweka msingi mzuri wa utekelezaji wake. 

Equinor ni moja ya wabia wakuu wa utekelezaji wa mradi huu wa LNG ambao utasimamiwa na Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA). Wabia wengine ni pamoja na kampuni ya Shell na TPDC kwa niaba ya serikali. 

Mradi wa LNG unakadiriwa kuwa wa thamani ya takriban Dola za Marekani bilioni 30 huku ukitarajiwa kutengeneza nafasi za ajira za moja kwa moja 6,000 na zisizo za moja kwa moja zaidi ya 15,000 kwa Watanzania.

Post a Comment

Previous Post Next Post