DKT. ABBAS ATOA ZAWADI KWA TIMU ZA WANAWAKE SHIMIWI

 

*************************

Na John Mapepele, Morogoro

Katibu Mkuu wa Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dkt. Hassan Abbasi ametoa zawadi kwa timu za wanawake zitakazoshinda kwenye michezo ya SHIMIWI mwaka huu kushiriki kwenye Tamasha kubwa la Michezo kwa Wanawake nchini lijulikanalo kama Tanzanite litakalofanyika mwakani.

Dkt. Abbasi ametoa zawadi hiyo leo Oktoba 23,2021mjini Morogoro wakati alipokuwa akitoa  hotuba yake kwenye ufunguzi wa SHIMIWI ambapo amesema michezo ni jambo  muhimu na lakimkakati ambalo linaweza kuitambulisha nchi duniani.

Aidha amesema michezo ni nguvu laini (soft power) ya Taifa na ametolea mfano nchi ya Brazil ambapo amesema inafahamika duniani kwa sababu ya michezo.

Amepongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa kupata  mafanikio makubwa ya michezo katika kipindi kifupi.

Ameyataja mafanikio hayo kuwa ni pamoja na Timu ya Taifa ya Mpira wa Miguu ya Wanawake (Twiga Stars) kutwa kombe la COSAFA baada ya kuzifunga timu za nchi zote za kusini mwa Bara la Afrika mwaka huu.

Pia amesema Timu ya Taifa ya Mpira wa Miguu ya wanawake chini ya Umri wa miaka 20 imebakiza mechi chache kufuzu  mashindano ya dunia,ambapo pia ameitaja  timu ya Kriketi  ya wanawake kuwa imekuwa mshindi wa tatu kwa Bara la Afrika.

Naye Mwenyekiti wa SHIMIWI Daniel Mwalusamba  ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Sanaa na Utamaduni kwa kuratibu mashindano haya ambapo amesema yamepata  mafanikio makubwa.

Akitaja  mafanikio hayo Mwalusamba amesema  hadi mwaka 2014 tayari wanamichezo 2584 walikuwa wameshiriki michezo hiyo ambapo amesema  michezo hiyo imesaidia kuondoa  matabaka  miongoni mwa watumishi wa Serikali kwani yamewafanya wanamichezo wa kada za chini na kada za viongozi kujumuikka na kucheza pamoja.

Ameongeza kuwa  michezo hiyo imesaidia kuibua vipaji ambapo hadi sasa imeweza kuzalisha  waamuzi waliofika kwenye ngazi ya FIFA, pia amesema michezo imetoa wachezaji wa netiboli katika ngazi ya kitaifa.

Kwa upande mwingine amesema  michezo hii inatoa motisha kwa kuwa watumishi wanapata  posho ambazo zinasaidia familia zao.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela ameiomba Serikali kuendelea kufanyia mashindano hayo katika mkoa wake  kwa kuwa upo katika ya nchi ambao unatoa fursa ya watumishi kutoka pande zote kushiriki.

Akijibu ombi hilo mgeni rasmi wa shughuli hiiMakamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.Dkt, Philip Isdor Mpango ameitaka Wizara yenye dhamana ya michezo nchini kulitafakari.

Post a Comment

Previous Post Next Post