WAKAGUZI WA MAZINGIRA FANYENI KAZI KWA BIDII NA UADILIFU-JAFO

 WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Selemani Jafo, amewataka Wakaguzi wa Mazingira kuwa waadilifu katika utendaji wa kazi zao ili kuhakikisha mazingira yanakuwa salama kwa manufaa ya Taifa. Amesema kuwa mara baada ya kupata mafunzo anauhakika kila mtu atafanya kazi kwa juhudi na uadilifu kulingana na mafunzo aliyopata.

Ameyasema hayo alipokuwa akifunga mafunzo ya Wakaguzi wa Mazingira yalioyofanyika katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete Jijini Dodoma, mafunzo ambayo yameandaliwa na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), kwa lengo la kukuza uelewa wa jinsi ya kufanya ukaguzi wa mazingira.

Aidha Mhe. Jafo amesema, kuwa mkaguzi wa mazingira ni jukumu kubwa sana katika kuhakikisha Tanzania inakuwa salama katika upande wa Mazingira, kwa mujibu wa Sheria ya Mazingira, Waziri wa Mazingira ana mamlaka ya kuteua Wakaguzi wa Mazingira katika Wizara pamoja na mamlaka za Serikali ili waweze kusimamia Mazingira sehemu husika kwa kumuwakilisha Waziri. 

“Nafasi ya kuteuliwa ni nafasi kubwa sana ambayo unapewa dhamana ya kukagua Mazingira sehemu yoyote kulingana na mujibu wa sheria na kanuni zake. Nimepewa mamlaka ya kuteua wakaguzi wa mazingira na hii imenisaidia ili kupata wakaguzi ambao nitafanya nao kazi kwa umahiri na kutekeleza kwa mujibu wa Sheria. Tutambue kuwa hatuwezi kuteua wakaguzi wa mazingira bila ya kupata mafunzo kujiridhisha kama wamefuzu katika ukaguzi wa Mazingira”

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazigira (NEMC) Dkt. Samuel Gwamaka, amesema kuwa wakaguzi wa mazingira wapo kwa mujibu wa sheria na kanuni ya mwaka 2006 ambayo sasa hivi imeshaboreshwa inasubiri Waziri kusaini. Ili kuweza kuwa Mkaguzi wa Mazingira ni lazima wapitishwe kweye sheria na kanuni hivyo mafunzo haya ni muhimu kupata kwa wakaguzi wote ili kufuzu wakati wa utekelezaji wa kazi zao.

“Nipende kusema kuwa Sheria ya Mazingira imegusa kila kitu kikubwa utekelezaji wake ambao kwa sasa una changamoto zake, ndio maana tunajitahidi kuendelea kuelimisha jamii kwamba watu wafate Sheria bila shuruti na pia kutambua wajibu wao katika kusimamia Mazingira. Japo tunatoa elimu kwa jamii lakini tunahitaji kuwa na Wakaguzi wa Mazingira ambao watasaidia kukagua na kuendelea kutoa elimu kwa jamii, kwa hiyo mafunzo haya yatawasaidia kufanya ukaguzi kwa mujibu wa sheria na kanuni za Mazingira.”


Dkt. Gwamaka amemaliza kwa kusema kuwa endapo mkaguzi wa mazingira atafanya kazi zake kinyume na maadili na mafunzo waliyopewa bila shaka hatua za kisheria zitachukuliwa juu  ya Afisa huyo. Mafunzo kwa wakaguzi wa Mazingira yamefungwa rasmi leo na Mhe. Selemani Jafo jijini Dodoma.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Selemani  Jafo, akizungumza na washiriki wa mafunzo ya Ukaguzi wa Mazingira yaliofanyika ukumbi wa Jakaya Kikwete Jijini Dodoma, ikiwa ni kilele cha mafunzo hayo. Kulia ni Mkurugenzi wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Dkt. Samuel Gwamaka pamoja na Mkurugenzi wa Utekelezaji na Uzingatiaji wa Mazingira NEMC Muhandisi Redempta Samwe.
Baadhi ya washiriki wa Mafunzo ya wakaguzi wa Mazingira wakisikiliza kwa makini maelekezo ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe.Selemani Jafo Jijini Dodoma
Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Dkt. Samuel Gwamaka akitoa salam ya ukaribisho kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe.Selemani Jafo baada ya kuwasili katika mkutano wa mafunzo ya Wakaguzi wa Mazingira jijini Dodoma.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe.Selemani Jafo akiwa katika picha ya Pamoja na washiriki wa mafunzo ya Ukaguzi wa Mazingira. Wapili kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Dkt. Samuel Gwamaka

Post a Comment

Previous Post Next Post