Mamlaka ya Majisafi na usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imeanza utekelezaji wa kazi ya kuongeza huduma ya maji katika maeneo ya Msakuzi hadi Makabe ,Kata ya Goba Wilaya ya Kinondoni Jijini Dar es Salaam.
Akiongea wakati wa zoezi hilo, Meneja uzalishaji na usambazaji DAWASA, Mhandisi Tyson Mkindi amesema zoezi linalofanyika ni kuongeza toleo la inchi 12 kwenye bomba kubwa la inch 24 eneo la msakuzi ambapo bomba litalazwa kwa umbali wa kilomita 1.4 litakalosaidia kuongeza kiwango cha upatikanaji huduma ya maji na kupunguza mgao wa maji uliopo.
"Kazi kubwa tunayoifanya ni kuongeza uzalishaji maji yatakayowahudumia wananchi wa Msakuzi na Makabe ambapo mtandao wa maji upo kwa sehemu kubwa lakin huduma ya maji kwa maeneo mengine ni mgao" aliongezea Mhandisi Mkindi
Kwa upande wake Meneja wa DAWASA Ubungo, Gilbert Masawe amesema takribani wananchi 5000 wanategemea kunufaika na huduma hiyo katika mitaa ya Msakuzi kusini, Kwa paulo, Kwa biligenda, Victoria Hill na baadhi ya maeneo ya Makabe" alimalizia ndugu Masawe
Mmoja wa wananchi wa Makabe , Peter Mfuko ameeleza kufurahishwa na zoezi hilo na kuitaka DAWASA kuharakisha kazi hiyo ili kuwapunguzia adha ya wananchi wanaopata maji kwa mgao na wale wasiokuwa na huduma zaidi.
"Huu mradi tuliahidiwa kama miaka mitatu nyuma, Tunaishukuru sasa serikali na DAWASA wameanza kutekeleza hivyo tunaamini utakamilika ndani ya muda muafaka na sisi wakazi wa msakuzi mapinduzi tutafaidika na mradi" aliongezea Ndugu Mfuko