Naibu Waziri Awataka Makandarasi Kurejesha Mikopo Kwa Wakati

 

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara akiwa kwenye picha ya pamoja na menejimenti na wafanyakazi wa Bodi ya Makandarasi (CRB) mara baada ya kufunga mkutano wa siku mbili wa mashauriano baina ya bodi hiyo na makandarasi wazalendo uliofanyika jijini Mwanza mwishoni mwa wiki.

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara akizungumza na viongozi wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB), mara baada ya kufunga mkutano wao wa mashauriano na makandarasi wazalendo jijini Mwanza. Kushoto ni Naibu Msajili Mhandisi David Jere, Msajili  wa Bodi Mhandisi Rhoben Nkori, mkandarasi Pastory Masota na Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Consolatha Ngimbwa.

Msajili wa Bodi ya Makandarasi (CRB), Mhandisi Rhoben Nkori (kulia) akiteta jambo na Mwenyekiti wa bodi hiyo, Mhandisi Consolatha Ngimbwa kulia na Naibu Msajili wa Bodi hiyo, Mhandisi David Jere mara baada ya hafla ya kufungwa kwa mkutano wa nne wa mashauriano na makandarasi wazalendo uliofanyika mwishoni mwa wiki jijini Mwanza.

Na Mwandishi Wetu, Mwanza
MAKANDARASI wametakiwa kurejesha kwa nidhamu fedha wanazokopa kwenye benki mbalimbali ili wajenge uaminifu na wengine waweze kukopa na kinyume chake ni kusababisha benki hizo kushindwa kuwaamini wengine

Hayo yamesemwa mwishoni mwa wiki na Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara, wakati akifunga mkutano wa nne wa mashauriano wa makandarasi kanda ya ziwa uliofanyika jijini Mwanza ulioandaliwa na Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB).

Amesema CRB imeanzisha mfuko ambapo makandarasi wazalendo wa madaraja yote wanaweza kukopa lengo ikiwa ni kuwajengea uwezo hivyo ukuaji wake utategemea sana uaminifu wa marejesho ya fedha zitakazochukuliwa.

Amesema serikali itaendelea kutenga miradi ya kuwajengea uwezo makandarasi wazalendo na amewataka kuonyesha uwezo kwa kukamilisha miradi watakayopewa kwa ubora wa hali ya juu na kwa wakati ili waendelee kuaminika kwa wateja.

Naibu Waziri pia ameipongeza CRB kwa kuandaa mikutano ya mashauriano na makandarasi akisema kuwa inawapa mwanya makandarasi hao kubadilishana mawazo na ujuzi na wenzao na kueleza changamoto mbalimbali zinazowakabili ili zitatuliwe.

“Nawapongeza kwa kuandaa mikutano hii kwani hapa ndipo mnajipanga kuinua makandarasi, mnakosoana mlipokesea na mnashauriana namna ya kwenda mbele kwa hiyo sisi serikalini tunaiunga mkono mikutano hii iendelee kwa sababu faida zake ni nyingi kwa washiriki na nyinyi bodi.” Alisema Waitara

Vile vile amewataka makandarasi wanaofanya kazi kwa ubia kuacha tabia ya kugawana faida kabla ya miradi wanayoifanya kukamilika kwani hali hiyo husababisha miradi mingi kutokamilika kwa wakati.

Amesema makandarasi wengi wazalendo wamekuwa wakikwama kutokana na tamaa ya fedha mara wanapopata miradi tofauti na wenzao wa China ambao hugawana faida baaada ya kumaliza kazi na wamekuwa wakijituma kutokana na kufuatiliwa na nchi yao.

“Nimetembelea miradi mingi hapa nchini nimekuta mingi sana wanafanya wachina kumbe ni kwasababu wanafanyakazi kwa uaminifu na hawagawani faida mpaka kazi iishe na kwao kuna sheria kali sana wakiharibu kazi huku ndiyo sababu wana nidhamu ya kazi kuliko sisi” amesema Waitara.

Amesema tamaa na ubinafsi umesababisha makandarasi wazalendo kushindwa kuungana ili wapate uwezo wa kimtaji na mitambo ya kutekeleza miradi mikubwa ya ujenzi kama ilivyo kwa wenzao wa China ambao hawaweki ubinafsi mbele.

“Kuna watu wakiungana wakipata malipo ya awali tu wanapanda ndege kwenda Dar es Salaam kugawana fedha hata kabla ya mradi kuanza sasa mkifanya hivyo na mradi ukasimama fedha za kuuendeleza mtazipata wapi." Alihoji Naibu Waziri

Aidha, Waitara aliongeza kuwa, hata kama makandarasi wataungana na kutekeleza miradi mikubwa wanapaswa kugawana faida kidogo na kuacha mtaji wa kuanzia iwapo watapata kazi zingine kwani wengi wao hushindwa kuanza miradi mipya wanayoipata.

“Kuna mtu wanashangaza sana unakuta mtu hata kazi hajafika nusu ameshanunua gari la kifahari, kamnunulia mke wake gari la kisasa mambo ya kushangaza kabisa, kwanini usisubiri ukamilishe mradi wa watu uwe na amani ya kutumia fedha zako.” Alisema Waitara

Post a Comment

Previous Post Next Post