BARABARA YA SANZATE – MAKUTANO KUKAMILIKA OKTOBA

 

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mheshimiwa Mwita Waitara, akijibu swali Bungeni, Jijini Dodoma.

…………………………………………………………………..

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhe. Mwita Waitara, amesema kuwa ujenzi kwa kiwango cha lami sehemu ya barabara ya Makutano – Sanzate (Km 50) unatarajiwa kukamilika mwezi Oktoba mwaka huu mara baada ya kupatiwa ufumbuzi changamoto zilizokuwa zikiukabili mradi huu.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri huyo Bungeni Leo Juni 7,2021 jijini Dodoma alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Bunda Vijijini, Mheshimiwa Boniphace Getere, lililouliza Je ni kikwazo gani kinazuia kukamilika kwa ujenzi wa barabara ya Makutano – Sanzate kwa kiwango cha lami ambayo ina miaka tisa sasa tangu kuanza.

“Kwa sasa kazi zilizobaki ni asilimia 12 ambayo kufuatana na mpango mpya wa ujenzi, Mkandarasi amepanga kukamilisha ujenzi ndani ya miezi minne kuanzia sasa”, amesema Waitara. 

Aidha, Waitara ameongeza kuwa hadi kufika sasa Mkandarasi ameshapeleka katika eneo la kazi vifaa muhimu vya ujenzi ikiwa ni pamoja na magari, kokoto na lami.

Waitara ametaja changamoto zilizokuwa zikikabili mradi huu kuwa  ni pamoja na upatikanaji wa changarawe kwa ajili ya tabaka la barabara (G45), kuongezeka kwa kiasi cha upasuaji miamba na kuongezeka kwa kiasi cha ukataji udongo, hali ambayo ilisababisha kubadilishwa kwa usanifu wa barabara na kulazimu Mkandarasi kuongezewa muda wa utekelezaji wa mradi hadi Februari 2021.

Waitara amesisitiza kuwa Serikali itamlipa mkandarasi mapema iwezekanavyo baada ya kuhakiki madai yake, kiasi cha Shilingi bilioni 1.7 anazodai ili kumrahisishia kukamilisha kazi za ujenzi zilizobaki.

Ujenzi kwa kiwango cha lami wa sehemu ya barabara kutoka Makutano hadi Sanzate yenye urefu wa kilometa 50, unatekelezwa na Mbutu Bridge JV Contractors ambayo ni Muungano wa Makampuni ya kizalendo kumi na moja kwa gharama ya Shilingi bilioni 46.1.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi.

Post a Comment

Previous Post Next Post