WASANII WA KIZAZI KIPYA KUPAMBA UMISSETA, UMITASHUMTA

 

Dkt. Hassan Abbasi, Katibu Mkuu wa Wizara ya
Habari,Utamaduni Sanaa na Michezo akifanya
Mahojiano  kwenye kituo cha Redio
cha Safari FM mjini Mtwara

…………………………………………………………………..

Na John Mapepele, Mtwara

Wasanii wa muziki wa kizazi
kipya, taarabu na singeli ni miongoni mwa makundi ya wasanii watakaopamba
Mashindano ya Michezo na Taaluma kwa Shule za Msingi Tanzania (UMITASHUMTA) na
Sekondari (UMISSETA) yanayofunguliwa leo Juni 08, 2021 na Waziri Mkuu, wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa kwenye
Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara

Katibu Mkuu wa Wizara ya
Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Hassan Abbasi, amebainisha hayo alipofanya
mahojiano na Vituo vya Redio mjini Mtwara leo ambapo amewataja wasanii wa
kizazi kipya watakaopamba mashindano hayo kuwa ni pamoja na Ibrah kutoka Konde
Gang, Beka Flavour, Peter Msechu na Linah Sanga, pia msanii maarufu wa Singeli Dulla
Makabila na Mfalme wa taarabu Mzee Yusuf.

Amesema mashindano ya mwaka
huu yanaanza leo na kumalizika Julai 3, mwaka huu, ambapo amesisitiza kuwa lengo
la Serikali kwa sasa ni kuendelea kuboresha na kuongeza baadhi ya michezo ambayo
itawasaidia kuweza wanafunzi wanapomaliza masomo yao kupata ajira.

“Tunakusudia kuangalia michezo
inayoweza kumwandaa kijana kupata ajira baada ya kumaliza shule. Michezo ya
maigizo ni miongoni mwa tasnia inakua kwa kasi kubwa hapa nchini ambayo kama mtoto
akiandaliwa  vizuri anaweza kujiajiri”
ameongeza Dkt. Abbasi

Amewataka wazazi kuondokana na
fikra potofu ya kwamba michezo haina maana kwa kuwa kwa sasa michezo ni uchumi
na ajira kubwa duniani.

Pia Dkt. Abbasi amesema katika
mashindano ya sasa wamevialika vilabu, vyama, na mashirisho mbalimbali kuja kuona
vipawa na vipaji vya wanamichezo hawa chipukizi

Mashindano hayo yatafanyika
katika Viwanja vya Nangwanda Sijaona, Chuo cha Walimu Mtwara (TTC kawaida),
Chuo cha Walimu ufundi Mtwara Ufundi Mtwara na katika Shule ya Sekondari ya
Ufundi Mtwara maarufu Mwasandube.

Post a Comment

Previous Post Next Post