WAFANYAKAZI WA I&M BANK WAJITOLEA DAMU KUOKOA MAISHA YA WATANZANIA WAKISHIRIKIANA NA HOSPITALI YA TAIFA YA MUHIMBILI

  

Meneja masoko na mawasiliano benki ya I&M Tanzania kushoto Bi.Anitha Pallangyo akiwa na wafanyakazi wenzie katika kampeni ya uchangiaji dau
         Damu ikiendelea kutolewa kutokana na hamasa iliyoletwa na wafanyakazi wa Benki ya I&M
    Bi.Lencer Odhiambo kutoka kitengo cha huduma kwa wateja cha benki ya I&M akiwa anajitolea damu katika kampeni ya kuchangia damu   
    Mkuu wa kitengo cha mikopo Bw.Clemence Kagoye wa benki ya I&M akiwa anatoa damu katika kampeni ya kuchangia damu ilioandaliwa na benki hiyo

Mwandishi Wetu

Benki ya I&M Tanzania, Ijumaa tarehe 30 Aprili 2021, walifanya Kampeni ya utoaji Damu ili kuokoa maisha ya watanzania chini ya mpango wao wa ‘IM FOR YOU’ katika jitihada za kurudisha kwa jamii. Kampeni hiyo ilifanyika Makao Makuu ya Benki hiyo yaliopo Maktaba Square jijini Dar es salaam.

Zaidi ya wafanyakazi 30 walishiriki na kujitolea Damu ili kuiwezesha Serikali kukabiliana na upungufu wa Damu kupitia hospitali ya taifa ya Muhimbili ambayo ilishirikiana na Benki hiyo katika zoezi la utoaji damu.

Kwasababu uhitaji wa damu bado upo, Benki ya I&M kupitia mpango wake wa ‘IM FOR YOU’ ambao wafanyakazi wake hujitolea kwa jamii wameamua kufanya kampeni hii ya uchangiaji damu kama njia ya kurudisha kwa jamii.

Akiongea wakati wa zoezi hilo la kujitolea damu, Bi. Anitha Pallangyo, Meneja Masoko na Mawasiliano wa Benki ya I&M alisema,”tumefurahishwa sana na muitikio ambao wafanyakazi wenzetu wameonyesha katika zoezi hili la kipekee. Tunawashukuru sana hospitali ya Taifa  Muhimbili kwa muitikio wao walioonyesha kwa kukubali kushirikiana nasi katika zoezi hili la utoaji damu ili kuokoa maisha ya watanzania wengi wenye uhitaji wa damu.”

 Kwa upande wake Meneja Mkuu wa Kitengo cha Uboreshaji huduma za Benki Bi. Deepali Ramaiya, , Alisema “Hii ni moja ya mipango mikakati ya aina yake ambayo huanzishwa  na wafanyakazi wenyewe wa Benki ya I&M, kwa kujitolea huduma bure kwa jamii kama vile kutoa Elimu ya Ujasiriamali bure kwa wafanyabiashara kupitia Vikundi mbalimbali na sasa wamejitolea damu kupitia Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

 Naye Afisa muhamasishaji damu kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili,John Daniel Bigambalaye alisema, “sisi kama wawakilishi wa Muhimbili kitengo cha damu, tumehamasika na kampeni hii iliyoandaliwa na wafanyakazi wa Benki ya I&M kwa jitihada hizi za kusaidia hospitali ya Taifa na watanzania wenye uhitaji wa damu kwa ujumla. Tunashauri na taasisi nyingine ziwe mstari wa mbele katika kuhamasisha wafanyakazi wake kujitolea kwa jamii”

 Benki ya I&M kupitia wafanyakazi wake wameweza kufanya kampeni mbalimbali za kusaidia jamii kama vile kujitolea kufundisha Wanawake, Vijana na Wajasiriamali, kujitolea damu  na mengine mengi kwenye sekta ya Afya, Elimu na Mazingira.

 Licha ya wafanyakazi wa Benki ya I&M kujitolea damu pia walialika Taasisi mbalimbali na kampuni zilizo karibu na Makao Makuu ya Benki ili kushiriki.

Post a Comment

Previous Post Next Post