UKUMBI MKUBWA WA KISASA KUPUMZIKIA ABIRIA WAZINDULIWA UWANJA WA NDEGE WA KIMATAIFA WA JULIUS NYERERE

 


Waziri wa Ujenzi na Uchuku Mhandisi Dk.Leonard Chamriho (wa tatu kulia) akishiriki ukataji keki kuashiria kuzinduliwa kwa ukumbi wa kupumzikia wageni wa Twiga Business Lounge uliopo kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Julius Nyerere Terminal III jijini Dar es Salaam.Wengine katika picha hiyo ni maofisa kutoka ATCL pamoja na Mwenyekiti wa Kamati ya Miundombinu ya Bunge Selemen Kakoso( wa pili kushoto).
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhandisi Dk.Leonard Chamriho (wa tatu kushoto) akiwa ameshika glasi ya Sampen pamoja na viongozi wengine baada ya kuzinduliwa kwa ukumbi huo.
Viongozi wa ATCL, baadhi ya wageni waalikwa wakiwa na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhandisi Dk.Leonard Chamriho wakiwa wamenyanyua juu glasi kama ishara ya kuzinduliwa rasmi kwa ukumbi huo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Ndege ATCL Mhandisi Ladslaus Matindi akizungumza wakati wa uzinduzi wa ukumbi wa kisasa wa kupumzikia abiria.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Dk.Leonard Chamriho akiwa na wageni wengine waalikwa wakati wa kuzinduliwa kwa ukumbi wa kupumzikia abiria katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Terminal III (aliyekaa mbele.)
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhandisi Dk.Leonard Chamriho akikata utepe kuashiria kuzinduliwa kwa ukumbi huo wa kupumzikia abiria uliopo katika uwanja huo.
Baadhi ya wageni wakishuhudia uzinduzi wa ukumbi huo.
 

Na Said Mwishehe, Michuzi TV

UKUMBI mkubwa wa kisasa wa kupumzikia wageni wa Twiga Business Lounge uliopo katika Uwanja wa Kimataifa wa Julius Nyerere Terminal III jijini Dar es Salaam umezinduliwa rasmi leo ukiwa na hadhi ya kimataifa.

Akizungumza leo jijini Dar  es Salaam wakati akizindua ukumbi huo, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhandisi Dk.Leonard Chamriho amesema Serikali imeamua kutoa kumbi hizo za abira kwa ajili ya kupumzikia pamoja na kuongezea tija na ufanisi katika usafiri wa anga , pia ATCL watazitumia vizuri kutangaza shirika hilo.

Hivyo ametoa rai  kwa ATCL kuendelea kuboresha na kukidhi viwango vya kimataifa."Tunasema hivi kwasababu Uwanja wetu huu wa Kimataifa wa Julius Nyerere unaotumiwa na kampuni nyingi za ndege kwa sasa, hivyo ni fursa yenu kutangaza biashara na kampuni hizo."

Ametumia nafasi hiyo kueleza Serikali itaendelea kuboresha majengo mengine ya abiria ikiwemo kumbi za kupumzikia ambapo ATCL wanategemewa kutoa huduma.

Ameongeza pamoja na kuwapa kumbi hizo Serikali itaendelea kufanya uchambuzi wa maeneo mengine kuona kama wakipewa wanaweza kuongeza tija na kushindana vema katika biashara hiyo.

"Nawapongeza ATCL kwa kuanza safari za China licha changamoto zilizopo kutokana na masharti mengi yanayotokana na udhibiti wa janga la Corona , ambayo mengi tunaendelea kuyafanyia kazi kwa ukaribu,"amesema .

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Miundombinu ya Bunge Selemani Kakoso pamoja na jitihada ambazo Seerikali imefanya yapo mambo ambayo yanahitajika kufanyiwa kazi , la kwanza ni kubeba sehemu ya madeni chechefu yanayoikabili ATCL.

"Madeni haya yatalifanya shirika hili lisiweze kufanya kazi iliyofikiriwa, naamini Serikali ikibeba yale madeni tutalifanya shirika letu liweze kusimama,"amesema Kakoso.

Awali akizungumza wakati wa uzinduzi huo   Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Ndege ATCL Mhandisi Ladslaus Matindi amesema mbali ya kuongeza mapato lakini na ubora wa huduma zao ni kiwango cha hali ya juu na kwamba ukumbi huo unaweza kuhudumia watu 200 kwa wakati mmoja na unahudumia mtu yoyote aliyetamani kutumia huduma zao kwa gharama nafuu kabisa.

 "Uwapo ndani unaweza kupata chakula , vitafunwa pamoja na vinywaji vya mbalimbali.Lakini ukumbi wetu utakuwa na sehemu ya watoto kwa ajili ya michezo,pia  tutakuwa na sehemu ambayo wafanyabiashara wanaweza kufanya kazi zao wakati akisubiri huduma zetu,"amesema.

Post a Comment

Previous Post Next Post