TIC YAANZISHA KITUO CHA MAWASILIANO KWA WAWEKEZAJI ILI KURAHISISHA UPATIKANAJI WA TAARIFA KWA WAWEKEZAJI

 Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu wizara ya uwekezaji Profesa Godius Kahyarara akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kufika katika Kituo cha uwekezaji kushuhudia utoaji huduma ya mawasiliano kwa Wawekezaji inayotolewa na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) leo Jijini Dar es Salaam. Mkurugenzi Mtendaji wa TIC, Bw.Maduhu Kazi akizungumza katika uzinduzi wa huduma ya mawasiliano kwa wawekezaji leo Jijini Dar es Salaam ambapo Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu wizara ya uwekezaji Prof.Godius Kahyarara alihudhulia kwaajili ya kushuhudia huduma hiyo inayotolewa na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC).  

Mkurugenzi Mtendaji wa TIC, Bw.Maduhu Kazi akieleza namna huduma ya mawasiliano kwa wawekzaji itakavyotumika mara baada ya kuzindua huduma hiyo leo Jijini Dar es Salaam, Kulia ni Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu wizara ya uwekezaji Prof.Godius Kahyarara.    

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu wizara ya uwekezaji Prof.Godius Kahyarara akipata picha ya pamoja na wadau mbalimbali wa Uwekezaji mara baada ya uzinduzi wa kituo cha mawasiliano kwa wawekezaji leo Jijini Dar es Salaam.Kulia kwake ni Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) Bw.Maduhu Kazi. Kushoto kwake ni Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF).

PICHA ZOTE NA EMMANUEL MBATILO

******************************

NA EMMANUEL MBATILO

Serikali kupitia Kituo cha uwekezaji Tanzania (TIC), imeanzisha kituo cha mawasiliano kwa wawekezaji ili kuwawezesha na kuwarahisishia wadau wa Uwekezaji kuweza kupata Taarifa mbalimbali wanazozihitaji kwa njia ya kupiga simu, E-mail na mitandao.

Akizindua kituo hicho leo jijini Dar es salaam Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu wizara ya uwekezaji Profesa Godius Kahyarara amesema taarifa zitakazopatikana katika kituo hicho ni pamoja na fursa za uwekezaji zilizopo nchini, Utaratibu wa kuwekeza,kupata leseni na vibali mbalimbali, Wawekezaji kupata taarifa za maendeleo ya maombi yao ya vibali na leseni yaliyowasilishwa TIC.

“Huduma hii itapunguza muda na gharama kwa wawekezaji ambapo badala ya kufika TIC watakuwa wanapata huduma ya kuwasiliana na TIC wakiwa mahali popote walipo ndani na nje ya nchi”. Amesema Prof.Kahyarara.

Aidha Prof.Kahyarara amesema kuwa faida ya Kituo cha mawasiliano kwa wawekezaji ni kupunguza muda na gharama kwa wawekezaji ambapo badala ya kufika TIC, Watakuwa wanapata huduma ya kuwasiana wakiwa mahala popote iwe ndani au nje ya nchi.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Sekta Binafsi nchini (TPSF), Bw.Zaki Mbena amesema kuwa Kituo hicho kitawasaidia wawekezaji ambao wengi wao wanatokea Sekta Binafsi kupata huduma kwa haraka zaidi popote pale walipo.

“Taasisi ya sekta binafsi Tanzania na wadau mbalimbali tumekuwa na mchango mkubwa katika kuboresha mazingira ya wawekezaji nchini lakini pia kuleta ufanisi kwa jinsi wawekezaji wanavyohudumiwa nchini”. Amesema Bw.Mbena.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa TIC, Bw.Maduhu Kazi amesema kwa kuanza kituo hicho kitatoa huduma ndani ya masaa 10 huku wakitarajia kuongeza masaa zaidi hapo baadae kutokana na mahitaji yatakavyokuwa.

Kituo cha mawasiliano kwa wawekezaji kitarahisisha kupata mrejesho wa huduma zinazotolewa na TIC na taasisi nyingine zinazotoka kwa wawekezaji.

Post a Comment

Previous Post Next Post