MBUNGE NEEMA LUGANGIRA AITAKA WIZARA YA KILIMO IJIKITE KATIKA PATO LA MKULIMA NA SIO BEI YA MKULIMA

 



Mbunge
wa Viti Maalumu kupitia Asasi za Kiraia Tanzania Bara (NGOs) Neema
Lugangira akisisitiza jambo wakati akichangia bajeti ya Wizara ya Kilimo
Bungeni Jijini Dodoma

Mbunge
wa Viti Maalumu kupitia Asasi za Kiraia Tanzania Bara (NGOs) Neema
Lugangira akisisitiza jambo wakati akichangia bajeti ya Wizara ya Kilimo Bungeni Jijini Dodoma

NA MWANDISHI WETU, DODOMA
Mbunge
wa Viti Maalumu kupitia Asasi za Kiraia Tanzania Bara (NGOs) Neema
Lugangira ameitaka Wizara ya Kilimo iache kuimba wimbo wa Bei ya Mkulima
badala yake watoke huko waende kwenye Pato la Mkulima ili kuongeza tija
kubwa kwenye sekta hiyo.
Aliyasema
hayo leo Bungeni Jijini Dodoma wakati akichangia Bajeti ya Wizara ya
Kilimo ambapo Mbunge Neema alisema kwa kipindi kirefu Wizarani wamekuwa
wakiongelea tu Bei ya Mkulima lakini wakati umefika sasa waongelee Pato
la Mkulima kwa sababu wanapoongelea Pato la Mkulima lina faida mbili ya
kwanza ni bei na ya pili ni wingi na ubora yaani kimahesabu Pato la
Mkulima lina Variables mbili = Price/Bei x (Quantity/Wingi +
Quality/Ubora). 
Alisema
kwamba Wizara ya Kilimo wamekuwa wakiweka jitihada kwenye Bei ya Mkulima
na sasa ameishauri Wizara ikumbuke hii Variable ya ya pili ya Q ambayo
ni Quanity/Wingi na Quality/Ubora.
Mbunge
Neema aliendelea kwa kusema kwamba kwa sababu Wabunge wengi wameongelea
tija yetu ya kwenye kilimo anapenda kutoa mifano miwili: Kwa wenzetu wa
Zambia wanauza kilo moja ya mahindi wanauza TZS. 250 mpaka 300 na
wakiuza kwa bei hiyo wanarudisha gharama zao yaani wamefikia break-even
point lakini kwetu sisi Tanzania ili kufikia kiwango cha break-even
lazima tuuze kilo moja ya mahindi TZS.500 .
“Hivyo
hivyo hata kwenye Pamba kwa nchi ambazo tunashindana nazo India,
Brazili, China , Egypt wao wanazalisha eka moja kilo 1,000 hadi 1,250 na
wao wakiingia sokoni wanaweza kuuza kwa bei ya TZS..500 kwa kilo na kwa
kiwango hiko wamekuwa wamefikia kiwango cha break-even lakini sisi kwa
sababu tija yetu ni ndogo tunazalisha eka hiyo hiyo moja kilo 250 hivyo
hatuwezi kuuza kwa bei ya TZS 500 yaani mpaka ifike angalau TZS 1000”
Alisema
Mbunge huyo
alipendekeza kwamba ifika wakati Wizara ya Kilimo ianze kuongelea Pato
la Mkulima na sio Bei ya Mkulima kwani kufanya hivyo wataweza kuongeza
tija ambayo itaongeza mchango wa Sekta ya Kilimo kwenye Pato la Taifa
kwa sababu wamekuwa wakisema asilimia 65 ya watanzania wapo kwenye
Kilimo lakini bado Sekta ya Kilimo inachangia asilimia 27 tu kwenye Pato
la Taifa. 
Mbunge
Lugangira alisisitiza kwamba kama Wizara itaendelea na Wimbo wa Bei ya
Mkulima basi itakuwa inaendelea kufidia upungufu wetu wa tija kupitia
Bei ya Mkulima jambo ambalo sio sahihi kwahiyo ni lazima sasa Wizara ya
Kilimo ijikite katika Pato la Mkulima.
Hata
hivyo pia Mbunge Lugangira aliishauri Wizara ya Kilimo ipitie upya
Vituo vya Rasilimali ya Kilimo Ngazi ya Kata “Ward Agriculture Resource
Centres” ione kama Vituo vinatumika kadiri ambavyo ilitakiwa na kama
kuna  changamoto virudishwe kuwa chini ya Wizara ya Kilimo ili viweze
kuchangia katika kukuza tija kubwa ya kilimo kama ilivyokusudiwa.
Kutokana
na kwamba Vituo hivyo vilikuwepo kwa miaka mingi na Halmashauri
zimekuwa hazitengi Bajeti ya Huduma ya Ugani jambo ambalo ni changamoto
kubwa katika uendelezaji wa kada hiyo muhimu kwa maendeleo ya kilimo
nchini.
“Kwanza
nakushukuru sana Mh Spika kwa kunipa nafasi ya kuchangia kwenye Bajeti
ya Wizara ya Kilimo na naomba nianza kwa kusema naunga mkono Hoja. Sera
ya Kilimo hapa nchini inasema Mgani mmoja Kijiji kimoja kama
tunavyofahamu kuna Vijiji takribani elfu 12000 na tuna Wagani elfu 7000
kwa sasa nchini hivyo tuna upungfu Wagani elfu  5000” Alisema
“Lakini
pia napenda kuipongeza Serikali kupitia Wizara ya Kilimo hususani
Waziri Profesa Adolf Mkenda na Naibu Waziri wake Hussein Bashe kwa
jitihada kubwa walizoweka kuleta Mageuzi kwenye Huduma za Ugani ikiwemo
kutenga Bajeti kwa ajili ya kuwanulilia Maafisa Ugani vitendea kazi kama
pikipiki, nawapongeza sana lakini bado kuna changamoto ambayo mimi
ninaiona na kwamba bado Wizara ya Kilimo inategemea Afisa Ugani huyo awe
mtaalamu kwa kila kitu ajue mazao yote, mbolea, wadudu,masuala ya
madawa, fangazi, ukungu na nk jambo ambalo sio rahisi” Alisema
Mbunge
Neema Lugangira alisema Serikali iliamua kuanzisha Vituo vya Rasilimali
ya Kilimo Ngazi ya Kata ili viweze kuwa na tija kubwa kwenye kilimo na
kama sikosei vituo hivyo vilianzishwa kwenye Kata 200 hapa nchini na
pamoja na kuanzishwa Serikali iliweka wataalamu kwenye vituo hivyo,
vitendea kazi kama kompyuta, Jenereta, screen za kufundishia nk,
“Katika
hili niwapongeze Wizara ya Kilimo maana nimeskia kupitia Hotuba ya
Waziri wa Kilimo Profesa Adolf Mkenda kwamba wanakwenda kufufua Vituo
hivyo lakini ningependa kushauri lazima Wizara ihakikishe Vituo hivyo
viweze kufanya kazi ambayo imekusudiwa kwa sababu hivi sasa Vituo hivyo
vipo chini ya Halmashauri kwenye Halmashauri nyingi vituo hivyo
havifanyi kazi iliyokusudiwa ya kuendeleza kilimo kwa mfano Kituo
kilichopo Chamwino badala ya kufanya kazi ya kuendeleza kilimo inatumika
na TARURA” Alisema.
Alisema
pia hawawezi kuendeleza Kilimo wakati hizo Halmashauri ambazo karibia
asilimia 70 ya Mapato yake ya Ndani yanatokana na Kilimo lakini Utengaji
wa Bajeti ya Huduma ya Ugani hawatengi na kwakuwa suala hili linahusu
Ofisi ya Rais TAMISEMI na Waziri yupo Bungeni anaskia  pengine
atawaambia wanapanga vipi kuhakikisha hizo Halmashauri zinatenga Bajeti
ya Huduma ya Ugani.
“Na
mimi naamini lengo zima la kuanzishwa Vituo hivyo ilikuwa ni kuhakikisha
wanaimarisha Huduma ya Ugani na wakifanya hivyo wataweza kuongeza tija
na muhimu zaidi kuongeza Pato la Mkulima.
Mbunge
Lugangira alimaliza kwa kusisitiza: “Kwa muda mrefu tumekuwa
tukiongelea Bei la Mkulima na kabla sijaingia hapa Bungeni nilikuwa
nafanya kazi kwenye Shirika ambalo lipo chini ya Wizara ya kilimo la
SAGCOT (Southern Agricultural Growth Corridor of Tanzania) kama
Mkurugenzi wa Idara ya Sera na nimefurahi nimemuona bosi wangu Mr.
Geoffrey Kirenga yupo kwenye Ukumbi wa Bunge kwa hiyo naendelea
kusisitiza Wizara ya Kilimo iache Wimbo wa Bei ya Mkulima na ijikite
katika Pato la Mkulima” Alisema

Post a Comment

Previous Post Next Post