WIZARA YA MADINI YAANZA KUSUKA MIKAKATI YA KUKUSANYA SH.BIL 650 MWAKA 2021/22

 

Siku moja tu baada ya Bajeti ya Wizara ya Madini kupitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Tume ya Madini imewasilisha wizarani Mapendekezo ya Mpango Mkakati wa Ukusanyaji Maduhuli ya Serikali ya shilingi Bilioni 650 kiasi ambacho Wizara imepangiwa kukusanya kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022.

Mapendekezo hayo yametokana na majadiliano ya kina yaliyofanywa na Tume ya Madini huku Maafisa Madini Wakazi kutoka Mikoa mbalimbali nchini wakishiriki kwa sehemu kubwa katika kuandaa mpango huo lengo likiwa ni kuhakikisha kwamba Wizara ya Madini inafikia lengo la makusanyo kwa mwaka husika.

Akizungumza katika kikao hicho, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Prof. Simon Msanjila ameelezea utayari wa Wizara kutekeleza mapendekezo hayo na kusema kuwa, mikakati hiyo itasaidia kufikia malengo ya makusanyo ikiwemo kusaidia maendeleo ya  ukuaji wa Sekta ya Madini nchini.

Aidha, ili kutekeleza mapendekezo ya mkakati huo, Prof. Msanjila ameunda Kamati Maalum ya kuishauri Wizara kuhusu namna bora ya kutekeleza mpango huo na kuitaka kamati kuyafanyia kazi haraka mapendekezo yaliyowasilishwa.

 ‘’ Nimepokea mapendekezo yote, mengi yanatekelezeka na mengine yanahitaji ushauri wa kitaalam. Kamati hii itayachambua mapendekezo yote na kazi hii ifanyike haraka. Vilevile, tayari nimezungumza na Chember of Mines (TCM) na wao watushauri,’’.

Aidha, katika kikao hicho, Prof. Msanjila ametumia fursa hiyo kuwashukuru na kuwapongeza Watumishi wote wa Wizara kutokana na mafanikio ambayo yamepatikana katika sekta na kueleza kuwa, yametokana na utendaji wa watumishi wote.

Akielezea mikakati ya kuendeleza watumishi wa Wizara ya Madini kitaaluma, Prof. Msanjila amesema kuwa Wizara imetenga fedha za kutosha kwa ajili ya watumishi wake kwa ajili ya elimu ya shahada ya uzamili (masters degree) katika vyuo mbalimbali ili kuhakikisha wanafanya kazi kulingana na sifa zinazohitajika.

Awali, akiwasilisha mapendekezo ya mpango mkakati huo, Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Tabora   Mayingi Makolobela, kwa niaba ya Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa, ameainisha mpango huo kuwa ni pamoja na kufanyika kwa maboresho kwenye Sheria ya Madini ili kwenye madini ujenzi  Broker waweze kutambuliwa kwa kuwa suala hilo litasaidia kuongeza usimamizi wa madini ya ujenzi  katika maeneo yote. ‘’ Pia, tunapendekeza wawepo Mawakala wanaoweza kusimamia madini ya ujenzi hata katika maeneo ya vijijini’’ ameongeza Makolobela.

Mapendekezo mengine ni pamoja na kuondolewa kwa  Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwa madini yanayoingizwa nchini ili kutoa fursa kwa kiwango kikubwa cha madini kuingizwa nchini na hivyo kuchochea biashara ya madini ikiwemo kuviwezesha viwanda vya kusafisha dhahabu vilivyojengwa kujiendesha vizuri.

Naye, Mwenyekiti wa Tume ya Madini Prof. Idris Kikula amesema kuwa, kabla ya kuja na mapendekezo hayo, timu ya wataalam ilipita maeneo mbalimbali nchini ili kuwezesha kutoka na mkakati unaotekelezeka utakaosaidia kuongeza mapato ya Serikali yanayotokana na Sekta ya Madini.

Kwa upande wake, Kamishna wa Tume ya Madini Janeth Lekashingo amesema kuwa, katika majadiliano yaliyofanyika, Maafisa Madini  walionesha ujuzi na uzoefu mkubwa ikiwemo dhamira ya kutaka sekta ya madini kuongeza tija kwenye pato la taifa.

Kikao hicho cha tarehe 30 Aprili, 2021, kimefanyika ikiwa ni utaratibu wa Wizara ya Madini kukutana na Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa  nchini  mara baada ya kuwasilisha bajeti yake ili kuweka mkakati wa pamoja wa namna ya kutekeleza majukumu na mipango kwa mwaka husika.

Post a Comment

Previous Post Next Post