…………………………………………………………………………………………….
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Selemani Jafo amewaasa vijana kuendelea kuuenzi Muungano kwa kudumisha amani nchini.
Jafo ametoa rai hiyo leo wakati akizungumza mara baada ya kuhudhuria Dua maalumu ya kumuombea aliyekuwa Rais wa kwanza wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) Hayati Sheikh Abeid Aman Karume iliyofanyika katika Ofisi za CCM Kisiwandui.
Amesema kuwa vijana wa sasa wanapaswa kuona fahari ya Muungano na kuyaenzi yale yaliyoachwa na Hayati Karume ambaye ameacha alama Zanzibar hususan katika ujenzi wa miundombinu na kuwajali wananchi.
Aliongeza kuwa kiongozi huyo alikuwa na maono makubwa kwa wananchi wake na kuweza kuwa mfano wa kuigwa kwa viongozi wengine hapa nchini na hata Afrika kwa ujumla.
“Tukumbuke kwamba Hayati Karume na Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere walifanya kazi kubwa ya kuasisi Muungano na leo hii tunajivunia kuwa Watanzania hivyo kwetu sisi ni faraja hatuna nchi nyingine isipokuwa ni Tanzania,” alisema.
Aidha Waziri Jafo alimpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa uongozi wake ambao umewafanya wananchi kuwa na Imani kubwa kwake.
Alitoa rai kwa Watanzania kwa ujumla kumuunga mkono kwa yale anayoendelea kuyatekeleza na kuwa ameonesha weledi katika utendaji wake ambao unaakisi aliyofanya Hayati Karume hasa katika ujenzi wa makazi bora kwa wananchi.
Aprili 7 ya kila mwaka ni kumbukumbu ya kifo cha Karume ambaye alifariki mwaka 1972 na Dua maalumu ya kumuombea imefanyika katika Ofisi za CCM Kisiwandui, Zanzibar ambapo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan na viongozi mbalimbali wameshiriki