Katibu Tawala msaidizi Uchumi na Uzalishaji mkoa wa Ruvuma Deogratius Sibula kushoto akimkabidhi cheti cha usajili wa Biashara mjasilimali mdogo Belinda Lyimo wakati wa mafunzo ya utoaji elimu ya usajili ya Biashara na makampuni yaliyotolewa na Wakala wa Usajili wa Biashara,leseni na Makampuni Brela yaliyofanyika jana mjini Songea.
Picha na Muhidin Amri
………………………………………………………………………….
Na Muhidin Amri,Songea
WAFANYABIASHARA wadogo na wakubwa mkoani Ruvuma,wametakiwa kusajili biashara zao ili ziweze kutambulika kisheria na kufungua wigo utakaosaidia kupata wateja wengi na mikopo kutoka katika taasisi za fedha.
Hayo yamesemwa jana na Afisa Msajili msaidizi wa Wakala wa usajili wa biashara na leseni(Brela) Swalehe Yahaya wakati akitoa elimu juu ya usajili wa majina ya biashara na makampuni kwa wafanyabiashara,wasindikaji chakula na watengenezaji bidhaa ndogo ndogo wa Manispaa ya Songea katika ukumbi wa Sido mjini Songea.
Alisema,elimu hiyo itawasaidia wafanyabiasha namna bora ya kusajili biashara zao,kujitangaza,kukuza na kulinda majina ya biashara zao ili kuepuka kuingiliwa na watu wengine.
Alitaja faida nyingine ya kusajili biashara inamwezesha kuomba zabuni kwenye taasisi za umma ambapo kutokana na sheria mpya ni vigumu kwa mfanya biashara asiyesajili biashara au kampuni yake kupata zabuni serikalini.
Baadhi ya wafanya biashara wamepongeza hatua ya Brela kutoa elimu hiyo kwani imefungua fursa ambayo itatangaza shughuli wanazofanya na uhakika wa kuuza bidhaa zao katika masoko mbalimbali ya ndani nan je ya mkoa wa Ruvuma.
Belinda Lyimo, ameishukuru Brela kuendesha mafunzo na kutoa elimu ambayo inakwenda kuwahamasisha kutengeneza bidhaa bora zenye uwezo wa kumudu kwenye soko la ushindani kuongeza idadi ya wateja ikilinganisha na apo awali ambapo licha ya kuzalisha bidhaa bora, lakini hazikutambulika na watu wengi.
Ambinga Swai alisema,elimu ya usajili wa biashara na makampuni iliyotolewa na Brela itawezesha wafanya biashara sio kutambulika tu bali hata kulinda majina yao yasitumiwe na watu wengine kujinufaisha.
Alisema, ni jambo jema kwa wajasiriamali na wafanya biashara kuweka mambo yao kisheria ili kulinda biashara zao,kuongeza idadi ya wateja na uhakika wa kupata zabuni kutoka kwenye taasisi za serikali.
Amewata wafanyabiashara, kuepuka kufanya shughuli zao kwa mazoea kwani tabia hiyo ndiyo inayo changia sana kurudisha nyuma juhudi zao licha ya kuzalisha na kuuza bidhaa zenye ubora wa hali ya juu.