Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila amesema kuwa katika kipindi cha mwaka 2020 Sekta ya Madini ilikua kuliko sekta nyingine huku ikiongoza pia kwa kuliingizia Taifa fedha za kigeni.
Profesa Msanjila ameyasema hayo leo tarehe 27 Aprili, 2021 kwenye ufunguzi wa kikao cha pili cha baraza la wafanyakazi wa Tume ya Madini ambalo linajumuisha Wajumbe kutoka Makao Makuu, Ofisi za Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa, Kamishna wa Kazi, Viongozi wa TUGHE ngazi ya Taifa, Mkoa na Tawi la Tume ya Madini.
Alisema kuwa, tangu kuanzishwa kwa Wizara ya Madini, mchango wa Sekta ya Madini kwenye Pato la Taifa umeendelea kukua kwa kasi na kusisitiza kuwa lengo la Wizara ni kuhakikisha mchango wa Sekta ya Madini kwenye Pato la Taifa unafikia asilimia 10 ifikapo mwaka 2025.
Alisema kuwa, Wizara ya Madini imeweka mikakati mbalimbali ili kuhakikisha wananchi wote wananufaika na rasilimali za madini ikiwa ni pamoja na kuongeza kasi ya utoaji wa leseni za madini kwa wachimbaji wadogo wa madini, ushirikishwaji wa watanzania kwenye sekta ya madini, wawekezaji kutoa huduma za jamii kwenye maeneo yenye shughuli za uchimbaji wa madini na uanzishwaji wa masoko na vituo vya ununuzi wa madini nchini.
Katika hatua nyingine, Profesa Msanjila akielezea mafanikio ya Sekta ya Madini, tangu kuanzishwa kwa Wizara ya Madini alisema kuwa kasi ya utoaji wa leseni imeongezeka ambapo katika kipindi cha mwezi Julai 2020 hadi Machi, 2021, Wizara kupitia Tume ya Madini ilitoa leseni za madini 8709 na uanzishwaji wa Ofisi za Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa na Maafisa Migodi Wakazi ili kusogeza huduma karibu na wananchi.
Profesa Msanjila aliendelea kutaja mafanikio mengine kuwa ni pamoja na uanzishwaji wa masoko ya madini 39 na vituo vya ununuzi wa madini 50 ili kuhakikisha wachimbaji wadogo wa madini wanapata masoko ya uhakika ya madini yao, kuimarika kwa udhibiti wa utoroshaji wa madini kupitia ujenzi wa ukuta wa Mirerani na kuimarisha ulinzi kwenye viwanja vya ndege na mipakani na usimamizi dhabiti wa mazingira kwenye shughuli za uchimbaji wa madini nchini.
Aidha, aliwapongeza watendaji wa Tume ya Madini wakiongozwa na Mwenyekiti wa Tume wa Madini, Profesa Idris Kikula, kwa usimamizi mzuri uliopelekea mafanikio ya Wizara ya Madini na kusisitiza kuwa Wizara ya Madini itaendelea kutatua changamoto zilizopo.
"Ninafahamu kabisa zipo changamoto zilizopo kwenye usimamizi wa Sekta ya Madini hususan kwenye ukusanyaji wa maduhuli, masoko ya madini na vituo vya madini vilivyoanzishwa, kama Wizara tunaendelea kuzitatua pamoja na kuweka mazingira mazuri ya kazi ikiwa ni pamoja na ujenzi wa Ofisi za Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa, ununuzi wa vifaa vya kazi na maboresho ya maslahi ya watumishi.
Naye Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula akizungumza kwenye ufunguzi wa baraza hilo alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa kuaminiwa na kuteuliwa tena kuendelea kuisimamia Tume ya Madini kwenye utekelezaji wa majukumu yake.
Aidha, aliishukuru Wizara ya Madini kwa maboresho ya ofisi za Tume ya Madini mikoani pamoja na ujenzi wa jengo la makao makuu ya Tume ya Madini jijini Dodoma ambapo ujenzi wake unatarajiwa kukamilika mapema Januari, 2022.
Naye Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba akizungumza kupitia mahojiano maalum na waandishi wa habari alieleza kuwa lengo la kikao cha pili cha baraza la wafanyakazi lilikuwa ni kujadili changamoto za utendaji kazi pamoja na kuzipatia ufumbuzi, kupitia bajeti kwa mwaka wa fedha 2021-2022 na kupewa mafunzo mbalimbali.
Aliongeza kuwa yeye kwa kushirikiana na menejimenti ya Tume ya Madini amejipanga kuhakikisha Sekta ya Madini inaendelea kukua kwa kasi kwa kufuata sheria na kanuni za madini kwa ubunifu na uzalendo wa hali ya juu.