WAZIRI MKUU AIPONGEZA DAWASA KWA KUWAFIKA WANANCHI NA VIWANDA

 Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,  Kassim Majaliwa ameipongeza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar-es-salaam (DAWASA) kwa jitihada zake katika kuboresha huduma kwa wananchi na maeneo ya Viwanda.


Waziri Mkuu ametoa pongezi hizo leo Aprili 27 katika ziara maalum ya kutembelea viwanda vilivyopo Wilayani Kibaha Mkoani Pwani.

"Nimesikia mikakati mizuri ya Mkoa wa Pwani, DAWASA, TANESCO na TARURA inayoleta matumaini makubwa katika kuboresha sekta ya Viwanda". Alisema Waziri Mkuu na kuongeza kuwa viwanda vina mchango mkubwa katika kuinua uchumi wa nchi na kuongeza mzunguko wa fedha katika jamii inayovizunguka.

Amesema kwa sasa sekta ya Viwanda na Uwekezaji ipo chini ya Ofisi yake na ametoa wito kwa taasisi wezeshi za Serikali kuweka mazingira bora ya kuvutia ili wawekezaji wakubwa na wadogo wawekeze mitaji yao.

Amesema viwanda vina faida nyingi kwa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla huku akitaja faida mbalimbali  zikiwemo ajira kwa vijana, upatikani wa vifaa kwa gharama nafuu, ukuaji wa pato la Taifa na ongezeko la mapato ya halmashauri.

Awali akitoa taarifa ya uboreshaji huduma ya Majisafi kwenye maeneo ya Viwanda,  Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA mhandisi  Cyprian Luhemeja amesema kuwa Mamlaka imejipanga kuboresha huduma za majisafi katika maeneo yake yote ikiwemo viwandani.  

"Waziri Mkuu, DAWASA inawekeza asilimia 40 ya mapato yake ya kila mwezi zaidi ya Tsh bilioni 13.5 kwa mwezi katika utekelezaji miradi. Jitihada ambazo zimewezesha DAWASA kufikia asilimia 92 ya wananchi ndani ya eneo lake la huduma," amesema.

Kuhusu eneo la viwanda la Zegereni, Wilayani Kibaha Mhandisi Luhemeja amesema tayari manunuzi ya mabomba yapo katika hatua za mwisho na kiasi cha Tsh bilion 1.6 kati ya bilioni.3.3 zinazohitajika kwa ajili ya ujenzi wa mradi huo zimepatikana.

Luhemeja ameishukuru serikali kwa kuendelea kuisaidia DAWASA na kumuahidi Waziri Mkuu uwajibikaji ili kutoa mchango stahiki katika kukuza uchumi wa nchi kupitia Viwanda.

Mhandisi Cyrian Luhemeja akitoa maelezo ya mradi mkubwa maji kuelekea eneo la Viwanda  la Zegereni wenye thamani ya zaidi ya Bilioni 3 utakaorahisha upatikanaji wa maji katika maeneo hayo na kuboresha huduma hiyo.

Post a Comment

Previous Post Next Post