NAIBU WAZIRI WA UJENZI AKAGUA BARABARA YA HAYDOM- MOGITU

 Mwandishi wetu, Manyara


NAIBU Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi mhandisi Godfrey Kasekenya amekagua barabara ya Haydom-Mogitu inayoungaanisha Wilaya za Mbulu na Hanang' Mkoani Manyara.

Akizungumza wakati akikagua barabara hiyo inayotarajiwa kujengwa kwa kiwango cha lami mhandisi Kasekenya amesema amelazimika kutembelea barabara hiyo ili wabunge wa eneo hilo wakizungumza juu ya changamoto za ubovu wa barabara awe anatambua.

Amesema barabara hiyo ya Haydom-Mogitu itajengwa kwa lami hivyo kuwarahisishia kusafiri wananchi wa eneo hilo.

Hata hivyo, Meneja wa Wakala wa barabara nchini TANROADS Mkoani Manyara, mhandisi Bashiri Rwesingisa amesema barabara hiyo itachepuka eneo dogo na kulipisha bwawa la Bassotu Wilayani Hanang' kuliko kujengwa pembeni ya bwawa.

Mkuu wa Wilaya ya Mbulu, Dokta Chelestino Simbalimile Mofuga amempongeza Naibu Waziri huyo mhandisi Kasekenya kwa kufika na kuona barabara zao kwani yeye ndiye huwa anajibu maswali Bungeni kwenye Wizara hiyo, hivyo anapaswa kutambua barabara zilivyo.

Mbunge wa Jimbo la Mbulu Vijijini mhe Flatei Gregory Maasay amemshukuru Naibu Waziri huyo mhandisi Kasekenya kwa kufika eneo hilo kwani ameona uhalisia wa barabara hiyo ulivyo.

Mkuu wa Wilaya ya Hanang' Ghaibu Lingo amesema wenyewe kama viongozi watapokea ushauri wa kitaalamu na kusimamia utekelezaji wa ujenzi wa barabara hiyo hasa eneo la Bassotu.

Mbunge wa Jimbo la Hanang' mhandisi Samwel Hhayuma amesema barabara hiyo ikijengwa kwa kiwango cha lami itasaidia usafiri kwa wananchi wa eneo hilo na wagonjwa wanaopelekwa hospital ya rufaa ya Haydom kupata matibabu.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Hanang' Rose Kamili Sukums amesema awali barabara ya kutoka Arusha hadi Singida ilikuwa inapita eneo hilo na kukatishia Bassotu.

Mkuu wa Wilaya ya Hanang' Mkoani Manyara, Ghaibu Lingo (kushoto) akizungumza wakati Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi mhandisi Godfrey Kasekenya (katikati) akikagua barabara ya Haydom-Mogitu, kulia ni Mbunge wa Jimbo la Hanang' mhandisi Samwel Hhayuma na viongozi wengine wa Wilaya ya Hanang'.
 
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi mhandisi Godfrey Kasekenya katikati akikagua barabara ya Haydom-Mogitu inayounganisha Wilaya za Mbulu na Hanang' Mkoani Manyara, kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Hanang' Ghaibu Lingo na kulia ni Mbunge wa Jimbo la Hanang' mhandisi Samwel Hhayuma, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Hanang'Rose Kamili Sukums na Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Hanang' Mathew Darema.

Post a Comment

Previous Post Next Post