MIRADI YA BARABARA ARUSHA YAKAMILIKA KWA SH. BILIONI 189

 ​Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Arusha Mhandisi Johnny Kalupale (kushoto), akielezea jambo kwa Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya wakati akikagua barabara ya mchepuko wa Kusini, maarufu kama Arusha Bypass (Kilometa 42.4). Wengine ni watumishi wa TANROADS mkoa wa Arusha.

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhandisi Godfrey Kasekenya, akitoa maelekezo kwa Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) mkoa wa Arusha Mhandisi Johnny Kalupale, wakati akikagua barabara ya mchepuko wa Kusini, maarufu kama Arusha Bypass (Kilometa 42.4). Wengine ni watumishi wa TANROADS mkoa wa Arusha.

************************

NA BALTAZAR MASHAKA, ARUSHA 

SERIKALI kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Arusha, imekamilisha miradi ya kitaifa ya ujenzi wa barabara zenye urefu wa km 82.5 kwa kiwango cha lami kwa gharama ya sh. bilioni 189.141.

Miradi hiyo ya barabara ya Sakina-Tengeru (njia nne) km 14.1, barabara ya mchepuko wa Kusini (Arusha Bypass) km 42.4  na ujenzi wa barabara ya Kia hadi Mererani na zote zimekamilika kwa asilimia mia moja.

Akitoa taarifa ya miradi hiyo jana kwa Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, Meneja wa TANROADS mkoani Arusha,Mhandisi Johnny Kalupale, alimweleza kuwa, barabara ya Sakina hadi Tengeru (njia nne), yenye urefu wa km 14.1 imegharimu sh.bilioni 70.365, barabara ya mchepuko wa kusini ya urefu wa km 42.4, imejengwa kwa gharama ya sh. bilioni 86.778 huku barabara ya Kia hadi Mererani yenye urefu wa km 26 ikigharimu sh. bilioni 32.

Alisema wakala huo unaendelea na usimamizi wa miradi ya ujenzi wa barabara za Mto wa Mbu-Loliondo (km.49), Kijenge-Usariver (km 20) na ujenzi wa mzani wa kisasa wa kupima uzito wa magari katika eneo la Kimokouwa katika barabara ya Namanga pamoja na kuendeleza ujenzi wa barabara ya njia nne kutoka Sakina hadi Tengeru (km 9.3).

Akizungumza na watumishi wa TANROADS mkoani Arusha jana baada ya kukagua barabara hizo Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya,aliwapongeza kwa kusimamia vyema miradi hiyo ya ujenzi wa barabara 

na kuhakikisha inakamilika kwa viwango vilivyoainishwa kwenye mikataba ya ujenzi, pia kuhakikisha barabara zote wanazozisimamia mkoani humo zinapitika majira yote ya mwaka.

“Nataka niwahakikishie kuwa, Serikali ya awamu ya sita chini ya  Rais wetu Mhe. Samia Suluhu Hassan, itaendelea kusimamia utekelezaji wa miradi yote ya uboreshaji wa miundombinu ya barabara iliyopo, lakini pia miradi mipya itakayotengewa fedha kwenye bajeti ya Serikali katika mwaka wa fedha wa 2021/2022, nayo itatekelezwa,” alisema Mhandisi Kasekenya.

Naibu Waziri huyo  alikuwa mkoani Arusha kwa ziara ya siku moja akitokea Dodoma kupitia barabara ya vumbi ya Kongwa kwenda Kibaya hadi Arusha (km 430), ambapo usanifu wa barabara hiyo umekamilika na ujenzi wake utatangazwa mara baada ya kutengewa fedha katika bajeti ya serikali kwa mwaka  huu wa fedha

Post a Comment

Previous Post Next Post