KATIBU MKUU ANDREW MASSAWE AKARIBISHWA RASMI WIZARA YA KILIMO

 Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Profesa Siza Tumbo akiwa pamoja na Wakuu wa Idara, Vitengo na Taasisi za Wizara ya Kilimo wakimpokea Katibu Mkuu Bwana Andrew Wilson Massawe leo tarehe 7 Aprili, 2021 katika Ofisi ndogo za Wizara ya Kilimo, Jijini Dar es Salaam mara baada ya kuteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan tarehe 4 Aprili, 2021.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Bwana Andrew Wilson Massawe akipewa maelezo na Naibu Katibu Mkuu Kilimo Profesa Siza Tumbo mara baada ya kuingia katika katika ofisi yake ndogo katika majengo ya Wizara ya Kilimo, Jijini Dar es Salaam.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Bwana Andrew Wilson Massawe akisaini kitabu maalum mara baada ya kuingia katika katika ofisi yake ndogo katika majengo ya Wizara ya Kilimo, Jijini Dar es Salaam.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Bwana Andrew Wilson Massawe akisaini kitabu maalum cha Wageni mara baada ya kuingia katika ofisi ya Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ubora wa Mbegu (TFRA) katika majengo ya Wizara ya Kilimo, Jijini Dar es Salaam.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Bwana Andrew Wilson Massawe akipokea nakara ya taarifa ya Taasisi ya TFRA kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu, Dkt. Stephan Ngailo katika ofisi za TFRA, Jijini Dar es Salaam.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Bwana Andrew Wilson Massawe akiongea na sehemu ya Watumishi wa Wizara ya Kilimo na Taasisi zake waliofika kumpokea na kumkaribisha kwa mara ya kwanza katika ofisi ndogo ya Wizara ya Kilimo, Jijini Dar es Salaam.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Bwana Andrew Wilson Massawe akiongea na sehemu ya Watumishi wa Wizara ya Kilimo na Taasisi zake (Hawapo pichani) waliofika kumpokea na kumkaribisha kwa mara ya kwanza katika ofisi ndogo ya Wizara ya Kilimo, Jijini Dar es Salaam.

***************************************

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bwana Andrew Wilson Massawe leo tarehe 7 Apriri, 2021 amekaribishwa rasmi katika ofisi za Wizara ya Kilimo, Jijini Dar es Salaam kufuatia uteuzi uliofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan tarehe 4 Aprili, 2021 ambapo aliteua Makatibu Wakuu, Naibu Makatibu Wakuu wa Wizara pamoja na Wakuu wa Taasisi mbalimbali.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Profesa Siza Tumbo aliwaongoza Wakuu wa Idara na Vitengo kadhaa wa Wizara kumpokea Katibu Mkuu Massawe katika ofisi ndogo za Wizara ya Kilimo (KILIMO I) Jijini Dar es Salaam ambapo baadae alipata nafasi ya kutembelea Mamlaka ya Udhibiti wa Ubora wa Mbolea (TFRA) na kisha kuzungumza na Menejimenti ya Taasisi hiyo.

Baada ya utambulisho kutoka kwa Viongozi kadhaa walioshiriki katika zoezi hilo pamoja na taarifa fupi ya Wizara ya Kilimo iliyotolewa na Naibu Katibu Mkuu Profesa Siza Tumbo na Mamlaka ya Udhibiti wa Ubora wa Mbolea (TFRA) ilitolewa na Mkurugenzi Mkuu Dkt. Stephan Ngailo.

Baada ya zoezi hilo kukamilia Naibu Katibu Mkuu Profesa Siza Tumbo alimpa nafasi Katibu Mkuu Andrew Massawe kuongea, ambapo alianza kwa kuwashukuru Viongozi waliojitokeza kumpokea na kumkaribisha

Katibu Mkuu Massawe alipongeza juhudi ambazo zimekuwa zikifanywa na Viongozi wa Wizara kuanzia Waziri, Naibu Waziri pamoja Wakuu wa Taasisi na Watumishi wote wa Wizara kwa kuendelea kuifanya Sekta ya Kilimo kuchangia katika uhakika wa chakula, lishe na kipato kwa Watanzania na kuongeza kuwa atakuwa tayari kujifunza.

Katibu Mkuu Massawe amesema anatambua kuwa kwa sasa Wizara ipo kwenye maandalizi ya mwisho ya uwasilishaji wa bajeti ya Wizara kwenye Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mwezi Mei, 2021 na kuongeza kuwa atajitahidi ili kuhakikisha anashirikiana na Viongozi wa Wizara pamoja na Watumishi wote ili Wizara iendelee kutoa matokeo chanya katika mambo yanayowalenga Wakulima na Watanzania wote.

“Naomba Watumishi wenzangu mnivumilie, tuwe tunaenda kwa mwendo wa matokeo na si kuongea tu.” Amekaririwa Katibu Mkuu Massawe.

Katibu Mkuu Massawe ameongeza kuwa jambo la pili atakalolifanya ni kuhakikisha kuwa Sekta Binfasi inayojihusisha na uzalishaji wa mbolea inagfanya kazi bega kwa bega katika kuwasaidia Wakulima wa Tanzania ila wafikiwe na pembejeo (Mbolea) kwa wakati na kwa bei nafuu.

Katibu Massawe amesema ni wakati muhafaka sasa Wizara kupitia Taasisi ya Utafiti wa Mazao ya Kilimo (TARI) kuanza kushirikia na Kampuni ya Mbolea ya Minjingu ili kupata matokeo bora ya mbolea zinazozalishwa na kiwanda hicho ili Wakulima wa Tanzania wapate mbolea bora kwa wakati na kwa bei nafuu.

Jambo lingine alilogusia Katibu Mkuu Massawe ni kuhakikisha kuwa Watumishi Viongozi wanaokaimu katika nafasi kadhaa; Wanadhibitishwa kutokana na sifa zao ndani ya Wizara ya Kilimo na Taasisi zake huku akiahidi kuanza kufuatilia mara moja suala la Watumishi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ubora Mbolea (TFRA) kukamilika kwa Muundo wa Taasisi (Scheme of Service) Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.

Katibu Mkuu Massawe amesema suala lingine ambalo anaona Wizara ya Kilimo inapaswa kulifanyia kazi kimkakati ni tozo na ushuru wa mazao ya Wakulima wa Tanzania katika Halmashauri kadhaa nchini.

“Nafahama juhudi hizi zimeanza kushughulikiwa na kimkakati na Wizara na kuongeza kuwa Naibu Waziri wa Kilimo Hussein Bashe ameunda timu maalum ya kulitazama suala hilo.”

“Niseme kuwa, tutalishughulikia kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kwa kuwaeleza faida zake na manufaa mapana zaidi ya Sekta ya Kilimo ili tuboreshe maisha ya Wakulima.” Amekaririwa Katibu Mkuu Massawe.

Jambo la lingine alilozungumzia Katibu Mkuu Massawe ni kuhusu suala la ununuzi wa mbolea kwa pamoja au Bulk Procurement System (BPS); Katibu Mkuu Massawe ameiagiza TFRA kufanya tathmini ya kina ili kushirikisha Vyama Vikuu vya Ushirika vingi ambavyo vitanza kuagiza mbolea hiyo kwa kiwango kikubwa kwa kushirikiana na Benki kadhaa zitakazokuwa tayari kutoa kinga katika ununuzi (Bank Guarantee).

Mwisho Katibu Mkuu Massawe amesema atapenda kuona Watumishi wa Wizara ya Kilimo wanatenda zaidi kuliko kuongea na kuwa na matokeo bora katika kazi zao za kila siku na kuongeza kuwa ili kuyapata matokeo bora suala la mawasiliano na mahusiano kati ya Watumishi wote ni lazima lijengwe na kuendelezwa.

“Niseme tu hauwezi kupata matokeo bora bila kuwa na mahusiano na mawasiliano mazuri; Hata kama utakuwa na rasilima watu ya kutosha pamoja na rasilimali fedha kama hakuna mahusiano na mawasiliano mazuri ni kazi bure.” Amemalizia Katibu Mkuu Massawe.

Post a Comment

Previous Post Next Post