KATAZO LA MIFUKO YA PLASTIKI LAFANIKIWA

 

Mkurugenzi Msaidizi wa Mazingira Bi. Kemilembe Mutasa akifungua Warsha ya wataalamu wa mazingira wa mikoa kuhusu utekelezaji wa marufuku hiyo pamoja na vifungashio vya plastiki visivyokuwa na viwango vya ubora na udhibiti wa taka za plastiki iliyofanyika Aprili 29, 2021 jijini Dodoma.

Mjumbe wa Kikosi Kazi cha Kazi cha Katazo la Mifuko ya Plastiki Bw. Sanford Kway kutoka Ofisi ya Rais-TAMISEMI akizungumza wakati wa Warsha ya wataalamu wa mazingira wa mikoa kuhusu utekelezaji wa marufuku hiyo pamoja na vifungashio vya plastiki visivyokuwa na viwango vya ubora na udhibiti wa taka za plastiki iliyofanyika Aprili 29, 2021 jijini Dodoma.

   

Washiriki wakiwa wakiwa katika Warsha ya wataalamu wa mazingira wa mikoa kuhusu utekelezaji wa marufuku hiyo pamoja na vifungashio vya plastiki visivyokuwa na viwango vya ubora na udhibiti wa taka za plastiki iliyofanyika Aprili 29, 2021 jijini Dodoma.

………………………………………………………………………………………

Utekelezaji wa marufuku ya utumiaji wa mifuko ya plastiki umefanikiwa kwa kiasi kikubwa katika kipindi chote cha takribani miaka miwili toka Serikali ilipotoa tangazo hilo.

Hayo yamebainishwa leo na Mkurugenzi wa Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt. Andrew Komba wakati akifungua Warsha ya wataalamu wa mazingira wa mikoa kuhusu utekelezaji wa marufuku hiyo pamoja na vifungashio vya plastiki visivyokuwa na viwango vya ubora na udhibiti wa taka za plastiki iliyofanyika leo Aprili 29, 2021 jijini Dodoma.

Katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Mkurugenzi Msaidizi wa Mazingira Bi. Kemilembe Mutasa alisema mafanikio hayo yametokana na ushirikiano wa Wizara, Taasisi mbalimbali, wananchi, waliokuwa wazalishaji na wasambazaji na makundi mbalimbali yaliyoshiriki katika kuzingatia maelekezo ya Serikali. 

Alisema pamoja na mafanikio haya yaliyopatikana, siku za hivi karibuni kumejitokeza changamoto ya matumizi ya vifungashio vya plastiki aina ya tubings kama vibebeo vya bidhaa mbalimbali na vilevile vifungashio hivyo kwa sasa vinazalishwa kwa wingi na kwa ukubwa tofauti. 

Aidha, alisema kuwa vifungashio hivyo vimekuwa vikitumika kama mifuko ya kubebea bidhaa sokoni na kuleta dhana kuwa mifuko ya plastiki iliyopigwa marufuku imerudi kivingine. 

Mkurugenzi huyo alibainisha kuwa vifungashio husika pia havikidhi viwango vya ubora vilivyoainishwa katika Mwongozo wa Viwango vya Ubora unaotolewa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kama Kanuni za Marufuku ya Plastiki za Mwaka 2019 zinavyoelekeza.

“Mifuko hii imeanza kuzagaa kwenye mazingira kwa kasi kubwa na hivyo kurudisha nyuma mafanikio makubwa tuliyoyapata katika kipindi chote cha kupambana na changamoto ya mifuko ya plastiki,” alitahadharisha.

Hata hivyo alisema kutokana na changamoto hiyo Serikali inaendelea kutoa elimu kwa umma kupitia vyombo vya habari, mitandao ya kijamii na kuelimisha umma kwa kuelekeza tofauti ya vifungashio visivyoruhusiwa na vinavyoruhusiwa kulingana na mwongozo wa viwango vya ubora.

Pia zoezi la kuhamasisha Wazalishaji na Wasambazaji wa vifungashio vinavyokidhi viwango vya ubora kuzalisha na kusambaza vifungashio hivyo kwenye masoko na maeneo ya biashara unaendelea.

“Kwa namna ya pekee nalishukuru Shirika la Dunia la World Wide Fund for Nature (WWF) kwa mchango wao wa kuhakikisha kuwa warsha inafanikiwa pamoja na masuala mbalimbali ambayo tumeendelea kushirikiana kuhakikisha mazingira yetu yanahifadhiwa na kusimamiwa ipasavyo,”

Post a Comment

Previous Post Next Post