Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Damas Ndumbaro akitoa hukumu ya Kitalu cha uwindaji cha cha Lake Natron East kilichoko wilayani Longido mkoani Arusha ambapo ameagiza kampuni ya Green Mile Safari irejeshewe leseni ya umiliki wa kitalu hicho iliyofutwa mwaka 2019.
Viongozi wa Kampuni ya Green Mile Safari wakiongozwa na Salim Balleith wakifuatilia hukumu ya Kitalu cha uwindaji chaK Lake Natron East kilichoko wilayani Longido mkoani Arusha iliyokua ikitolewa Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Damas Ndumbaro ambapo kampuni hiyo imerejeshewa leseni ya umiliki wa kitalu hicho.
Naibu Kamishna wa Uhifadhi Utalii na Huduma za Biashara, Imani Nkuwi kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) na Afisa Sheria kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Fredrick Komba (kushoto) wakifuatilia hukumu ya Kitalu cha uwindaji cha cha Lake Natron East kilichoko wilayani Longido mkoani Arusha iliyokuwa ikitolewa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Damas Ndumbaro leo jijini Dodoma.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Allan Kijazi akizungumza kabla ya kutolewa kwa hukumu ya Kitalu cha uwindaji cha cha Lake Natron East kilichoko wilayani Longido mkoani Arusha leo jijini Dodoma.
*********************************
Na Mwandishi Wetu – Dodoma
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Damas Ndumbaro ametoa hukumu ya Kitalu cha uwindaji cha cha Lake Natron East kilichoko wilayani Longido mkoani Arusha na kuagiza kampuni ya Green Mile Safari irejeshewe leseni ya umiliki wa kitalu hicho iliyofutwa mwaka 2019.
Akitoa maamuzi hayo Dkt. Ndumbaro amesema kitalu hicho kinarejeshwa kwa Kampuni hiyo hadi mwaka 2022 kufuatia kufanyika kwa maombi ya mapitio ya hukumu iliyoifanya Kampuni ya Green Mile ifutiwe umiliki wa kitalu hicho.
Aidha,Dkt. Ndumbaro amesema kufuatia uchambuzi uliofanyika kuhusu uamuzi wa kufutiwa umiliki wa kitalu cha Lake Natron – East, amejiridhisha kuwa malalamiko ya muomba mapitio ambayo ni kampuni ya Green Mile Safari yana msingi wa kisheria, na barua ya Mhe. Waziri ya kufuta umiliki wa kitalu haikuzingatia sheria na misingi ya utawala bora
“Iandaliwe rasimu itakayotumiwa katika umilikishaji wa vitalu itakayoonesha masharti ya kufuata ‘Terms and condition’ za kufuatwa na wawekezaji wakati wote wa umiliki wa kitalu cha uwindaji na kuwepo kwa umakini wakati wa kuandika nyaraka za kiofisi, ili kujiepusha na ukinzani wa sheria na taratibu zilizopo”, amesisitiza Dkt. Ndumbaro
Waziri Ndumbaro ameiagiza Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) iweke utaratibu wa kushughulikia migogoro haraka pindi inapojitokeza kuepusha hali iliyojitokeza.
Amesema mgogoro huo ulizorotesha ustawi wa uhifadhi na biashara ya Utalii, kuchafua taswira ya Tanzania katika tasnia ya uwindaji wa kitalii na kupunguza michango maendeleo kwa wananchi hivyo ni vyema TAWA ikahakikisha kuwa sheria, kanuni na miongozo inazingatiwa katika kusimaia sekta ya uwindaji wa kitalii.
“ Naishukuru Kamati ya ushauri kwa kazi nzuri waliyoifanya kwa kunishauri katika kufikia uamuzi wa suala hili kwa mujibu wa kifungu cha 38(15) cha Sheria ya Wanyamapori Na.5 ya mwaka 2009. Mtu yoyote ambaye hajaridhika na uamuzi huu, ana haki ya kukata rufaa kwa mujibu wa kifungu cha 38(16) cha Sheria ya Wanyamapori Na.5 ya mwaka 2009”.
Katika hatua nyingeine Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Ndumbaro amewaagiza viongozi wa Mkoa wa Arusha na Wilaya ya Longido kusimamia maamuzi ya Serikali katika suala hilo la kurejeshwa kwa leseni ya Kampuni ya Green Mile Safari katika Kitalu cha uwindaji cha Lake Natron – East.
Kabla ya kutoa uamuzi huo Dkt. Ndumbaro alifanya ziara katika eneo la kitalu hicho na kuzungumza na wananchi ambapo alijionea hali halisi ya kitalu chicho na rasilimali zilizopo katika eneo hilo la Kitalu pia alisikiliza pande zote zinazoguswa na mgogoro huo kabla ya kutoa uamuzi wake