WATU WANNE WANASHIKILIWA NA JESHI POLISI KWA KUTOROSHA VINYONGA NA NYOKA

 

Waziri w Maliasili na Utalii Dk. Damas Ndumbaro akizungumza na wanahabari mkoani Iringa hawapo pichani Leo katika ofisi za utalii mkoa wa Iringa.( Picha na Denis Mlowe)

****************************************

NA DENIS MLOWE,IRINGA

WAZIRI wa Maliasili na Utalii Nchini, Dk. Damas Ndumbaro amesema kuwa jeshi la polisi nchini linawashikilia watu wanne kwa kukamatwa na vinyonga 74 na nyoka sita waliowatorosha hadi nchini Austria.

 

Dk. Ndumbaro alisema hayo wakati akizungumza na wanahabari mkoani hapa, kuwa mtuhumiwa wa kwanza jina lake hakutaka kutaja kutokana na uchunguzi bado unaendelea alikamatwa nchini Austria  na kuhifadhiwa katika hifadhi ya wanyama ya Schonbrunn nchini humo.

 

Alisema kuwa serikali baada ya kupokea taarifa za kukamatwa kwa mlanguzi huyo wa wanyama walifanya uchunguzi ambao umefika asilimia 75 na kubaini kwamba vinyonga hao wametoka nchini Tanzania katika milima ya Usambara

 

Alisema kuwa kutokana na uchunguzi huo watanzania  hao wanne walikiri kuwauza vinyonga hao kwa wazungu wawili raia wa Chzech ambao pia majina yao hajayataja kutokana na kuendelea na uchunguzi zaidi.

 

Alisema kuwa wizara ina wasiwasi kwamba inawezekana biashara hiyo imefanyika kabla ya tukio hilo kujulikana na wanatarajia kufikishwa mahakamani kesho.

 

Dk. Ndumbaro alisema kuwa hadi sasa wamegundua wanunuzi hao waliingia nchini lini, walilala hoteli gani na walitumia pasi ya kuingilia na watu waliowapokea wazungu hao walipoingia nchini.

 

Alivipongeza vyombo vya ulinzi na usalama kwa kufanya kazi nzuri katika kuchunguza sakata hilo ambapo wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa sana kugundua njia mbalimbali zilizotumika na bado wanaendelea kufanya uchunguzi kuweza kubaini vinyonga haowalisafirishwa vipi kwenda nje Tanzania.

 

 Aliwaomba sana watanzania kuelewa kwamba Mei  2016 Serikali ilipiga marufuku biashara ya kukamata na kusafirisha wanyamapori  hai kwenda nje ya nchi lakini baada ya sitisho hilo kuna baadhi wanaendelea kufanya biashara hiyo haramu.

 

Alisema vitendo hivyo ni sawa na watu hao kuvunja sheria na kukabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi, rushwa na utakatishaji fedha kutoakana na mzunguko uliopo katika biashara hiyo kutokana na fedha inayotoka mlango wa nyuma na kutoa wito kwa watanzania kuacha mara moja kufanya hivyo.

 

“Ni kosa kubwa sana kisheria ni uhujumu uchumi, rushwa hivyo nawaomba watanzania wajue kuwa maliasili na wanyamapori ni rasimali kubwa nchini hivyo kitendo kinachofanywa na baadhi yetu ni kosa kubwa hapa na wakumbuke kuwa huo ni uhujumu uchumi kwani kuna watalii wanakuja kutokana na maliasili hizo kitendo cha wengine kukiuka ni uvunjaji wa sheria” alisema

 

Waziri Dk. Ndumbaro ametoa wito kwa Watanzania kuanza kampeni ya rasmi ya kutangaza maliasili na vivutio vilivyoko nchini Tanzania kwenye mitandao yao kwa kila mmoja ikiwe ni kuonyesha uzalendo nchini.

Alisema kuwa tuko takribani watanzania milioni 60 na endapo watanzania milioni 30 wakituma picha ya Mlima Kilimanjaro kwenye page zao au kivutio chochote kila mmoja kutokana na wafuasi wao wanaowafatilia ndani na nje ya nchi kiwango cha utalii kitaongezeka na kuwafanya watu mbalimbali wasioijua Tanzania vyema kuanza kuijua.

Alisema kuwa endapo kila mmoja kwa mfanoa akichukua picha ya mlima Kilimanjaro na kuandika mlima huu uko nchini Tanzania itakuwa kampeni kubwa ya kuabarisha dunia na kuwa njia ya kizalendo ya kuitangaza Tanzania kwa watanzania wenyewe kwa kutumia kurasa zao za mitandao ya kijamii.

Post a Comment

Previous Post Next Post