Dkt Nzuki Akaguaa Ujenzi Barabara Ya Seneto Hadi Kreta Ya Ngorongoro .

 Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt. Aloyce Nzuki leo tarehe 10 Machi, 2021 ametembelea Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro na kukagua ujenzi wa barabara ya Seneto hadi Kreta ya Ngorongoro yenye urefu wa Kilomita 4.4 inayojengwa kwa teknolojiaa ya mawe.


Dkt Nzuki ameipongeza Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) kwa uamuzi wa kutumia wataalam wa ndani kujenga barabara hiyo kwa kutumia teknolojia ya kiwango cha mawe ambayo ni nafuu na teknolojia rafiki hasa kwenye maeneo yenye milima na miteremko.

“Nawapongeza kwa ubunifu huu wa kutumia teknolojia ya ujenzi wa barabara ya mawe, na lazima tuishukuru Serikali kwa kutupa fedha za ujenzi wa barabara hii muhimu katika utalii, naamini itasaidia sana wageni wanaokwenda Kreta ya Ngorongoro hasa kwa kuzingatia kuwa eneo hili lina mteremko mkali kwa watalii wanapoelekea kwenye bonde la Ngorongoro” Alisema Dkt nzuki.

Dkt. Nzuki ameelekeza uongozi wa Mamlaka hiyo kuhakikisha mradi huo unatekelezwa kwa kasi na kukamilika ndani ya wakati uliopangwa kwa kuzingatia gharama halisi za ujenzi huo.

Naibu kamishna wa Uhifadhi wa NCAA (Huduma za Shirika) Bw. Audax Bahweitima amemueleza Katibu mkuu kuwa ujenzi wa barabara hiyo ni sehemu ya Mkakati wa NCAA kuboresha miundombinu ya barabara za ndani ya eneo la Hifadhi ili kuboresha huduma kwa wageni wanaotembelea hifadhi hiyo.

Bahweitima amefafanua kuwa katika utekelezaji wa mradi huo wamehakikisha kuwa ajira zinanufaisha wananchi wanaoshi ndani ya eneo la Ngorongoro na kuongeza kuwa hata uzalishaji wa malighafi kama mawe ya ujenzi yanayopatikana Wilayani Karatu yanatengenezwa na wakazi wa eneo hilo ikiwa ni Mkakaati wa Serikali kuhakikisha kuwa miradi ya ujenzi inawanufaisha wazawa kupata ajira.

Kwa upande wake Kamishna msaidizi Mwandaamizi (Huduma za Uhandisi) Mhandisi Daniel Chegere ameeleza kuwa ujenzi wa barabara hiyo unatarajiwa kugharimu kiasi cha shilingi Bilioni 2.6 na unatarajiwa kukamiliaka katika kipindi cha mwaka mmoja.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt. Aloyce Nzuki (kulia) akitoa maelekezo kwa Naibu Kamishna wa Uhifadhi wa NCAA (Huduma za Shirika) Bw. Audax Bahweitima (Katikati) kuhakikisha kuwa ujenzi wa barabara ya Seneto kuelekea Kreta ya Ngorongoro yenye urefu wa Kilomita 4.4 inakamilika katika muda uliopangwa na kuzingatia ubora katika ujenzi huo, Kushoto ni Kamishna Msaidizi mwandamizi (Huduma za Uhandisi) Eng. Daniel Chegere.
katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt Aloyce Nzuki (Kulia) akiwa pamoja na Naibu Kamishna wa NCAA (Uhifadhi, Utalii na Maendeleo ya jamii) Dkt. Christopher Timbuka (Kushoto) na Kamishna Msaidizi Mwandamizi (Huduma za Uhandisi) Eng. Daniel Chegere (katikati) wakati wa ziara ya kukagua ujenzi wa barabara ya Seneto.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt. Aloyce Nzuki (Kulia) akimzikiliza Mhandisi Daniel Chegere (Katikati) kuhusu ubora wa barabara zinazojengwa kwa mawe hasa katika maeneo yenye asili ya milima.
Muonekano wa barabara ya kutoka Geti la Seneto kwenda Kreta ya Ngorongoro yenye urefu wa Kilomita 4.4 ambayo imeanza kujengwa kwa kutumia teknolojia ya mawe.
Ujenzi wa kingo za Barabara ya Seneto kwenda Kreta ya Ngorongoro ukiendelea kabla ya hatua ya kupanga mawe kuanza.

Post a Comment

Previous Post Next Post