WAKANDARASI WATAKIWA KUTEMBELEA ENEO LA MRADI KABLA YA KUJAZA ZABUNI

 

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Dkt. Leonard Chamuriho, akitoa taarifa ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya Wizara yake kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, jijini Dodoma.

Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu ambaye ni Mbunge Jimbo la Singida Mashariki Mheshimiwa Miraji Mtaturu, akichangia hoja wakati wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi ikiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa Kamati hiyo, jijini Dodoma.

Muonekano wa ujenzi wa nyumba za makazi za Magomeni Kota zinazojengwa na kusimamiwa na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) ambao ujenzi wake umefikia asilimia 91, jijini Dar es Salaam.

Muonekano wa ujenzi wa Daraja jipya la Selander lenye urefu wa kilometa 1.03 ambalo linapita katika Bahari ya Hindi kuunganisha eneo la Agha Khan pamoja na Coco Beach umefikia asilimia 70.6.

…………………………………………………………………………………………

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhandisi Dkt. Leonard Chamuriho amewataka wakandarasi wote wanaoomba kazi za ujenzi wa miradi ya barabara kuhakikisha wanatembelea eneo la mradi kabla ya kujaza vitabu vya zabuni ili kuwawezesha kuweka gharama halisi ya mradi husika.

Dkt. Chamuriho ameyasema hayo jijini Dodoma, wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayosimamiwa na Wizara hiyo iliyotengewa fedha kwa mwaka wa fedha 2020/21 na itakayokaguliwa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu ambapo pamoja na mambo mengine Wizara imeelezea mafaniko yaliyopatikana kwa mwaka huo wa fedha na mikakati yake ya baadae.

“Kumekuwa na tabia za wakandarasi kutotembelea eneo la mradi na kuona fursa na changamoto zilizopo kabla ya kujaza vitabu vya zabuni hivyo kupelekea kuweka gharama isiyo halisi na kufanya miradi mbalimbali ya maendeleo kuchelewa kwa visingizio vya ukosefu wa malighafi za ujenzi”, amefafanua Dkt. Chamuriho.

Aidha, amewataka wakandarasi kuacha tabia ya kunakili gharama zilizotumika katika miradi mingine au zabuni zilizotekelezwa sehemu nyingine kwa kuwa gharama za ujenzi kwa kila mradi hutofautiana kulingana na maeneo husika.

Katika kuhakikisha fedha zinabaki nchini, Dkt. Chamuriho ameeleza kuwa Wizara imeendelea kuwashikiza wataalam wa ndani katika ujenzi wa barabara, madaraja na viwanja vya ndege kwa ajili ya kupata ujuzi ili waweze kusimamia miradi mikubwa ya ujenzi inayoendelea hapa nchini. 

 “Tunaendelea kuwajengea uwezo kwa kutumia taasisi zinazowasimamia kwa lengo la kuwainua wakandarasi wazawa ili waweze kunufaika na miradi inayotekelezwa katika nchi yetu”, ameongeza Waziri huyo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mheshimiwa Selemani Kakoso, ameitaka Wizara hiyo kuendelea kusimamia miundombinu inayojengwa kwani Serikali inatumia fedha nyingi katika ujenzi wake hivyo wahakikishe inatunzwa na kudumu kwa muda mrefu. 

“Hakikisheni mnawachukuliwa hatua stahiki wananchi wanaokiuka utaratibu ili kuweza kukomesha tabia ya watu kuharibu miundombinu hiyo ambayo imegharimu fedha nyingi za Serikali”, amesema Kakoso.

Ameipongeza Wizara kwa uzalishaji wa ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja zinazotokana na utekelezaji wa miradi ya maendeleo kama vile ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) kwa awamu zote, miradi ya ujenzi wa barabara, madaraja, vivuko, majengo ya Serikali na viwanja vya ndege.

Aidha, wajumbe wa kamati wameiomba Wizara kuendelea kutoa elimu kwa umma kupitia vyombo vya habari, vipeperushi, mikutano na semina kuhusu Sheria ya Barabara Na. 13 ya mwaka 2007.

“Wananchi wanahitaji kuelimishwa kuhusu hifadhi za barabara na kutofanya shughuli za kijamii kandokando ya barabara na kutopitisha mifugo sehemu ambazo sio maalumu kwa mifugo hiyo.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu inatarajia kuanza ziara ya kutembelea baadhi ya miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Wizara hiyo hivi karibuni, ambapo kwa ujumla kamati hiyo itatembelea mradi wa reli ya kisasa (SGR), uboreshwaji wa Bandari, Chuo cha Ujenzi cha Morogoro, mradi wa Magomeni Kota, Ujenzi wa Daraja jipya la Selander pamoja na mradi wa ujenzi wa barabara za Mabasi Yaendayo Haraka  (BRT), jijini Dar es Salaam. 

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi.

Post a Comment

Previous Post Next Post