TAFITI ZA USHIRIKA KULETA SULUHU YA CHANGAMOTO ZA USHIRIKA

 Tafiti za Ushirika zikitumika ipasavyo zimetajwa kuwa zinaenda kuongeza kasi na chachu ya maendeleo katika utatuzi wa Changamoto zilizopo katika Sekta ya Ushirika nchini.


Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Prof. Sizya Tumbo, akifungua Kongamano la Kwanza la Tafiti za Ushirika linalofanyika kuanzia Machi 16 -18, 2021, Jijini Dodoma.

Akifungua Kongamano hilo Naibu Katibu Mkuu ameeleza Tafiti mbalimbali zinazofanywa na Taasisi pamoja na Wadau kuwa kwa sasa bado hazijatumika ipasavyo kwani nyingi zimekuwa zikichapishwa na pengine kuhifadhiwa kwenye maktaba tu. Hivyo, kutofahamika na kuwanufaisha wanachama na wadau katika Sekta ya Ushirika.

“Lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa Vyama vya Ushirika vinanufaika na matokeo ya Tafiti zinazofanywa na wadau mbalimbali ili kuinua utendaji na kuondoa changamoto zinazoikabili Sekta ya Ushirika,” alisema Naibu Katibu Mkuu

Akieleza Malengo ya Kongamano hilo Mrajis wa Vyama vya Ushirika nchini,,Dkt. Benson Ndiege na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika amesema Kongamano la Tafiti za Ushirika linalenga kuwakutanisha wadau, watafiti na wanaushirika ili kujadili namna bora ya kuboresha Sekta ya Ushirika kupitia tafiti zinazofanyika kupitia maoni na mapendekezo yanayotolewa pamoja na uzoefu katika Sekta ya Ushirika.

Dkt. Benson Ndiege amezitaja baadhi ya Changamoto zinazoikabili Sekta hiyo ni pamoja na Ushirika kutokidhi mahitaji ya Wanachama, ukosefu wa mitaji, uongozi mbovu, ubadhilifu, elimu duni ya Ushirika. Akiongeza kuwa ni wakati muafaka sasa kwa wadau wote wa Ushirika kushirikiana kwa pamoja kutatua changamoto za Ushirika ili kuimarisha na kuongeza kasi ya maendeleo ya Ushirika.

Aidha, Mrajis amefafanua kuwa Tume ya Maendeleo ya Ushirika ina malengo makuu ya kuhakikisha kuwa Wanachama wa Ushirika wanakuwa uelewa pamoja uweledi wa kutosha katika Ushirika, uongozi na uwajibikaji katika Vyama vya Ushirika, kuwa na Vyama imara vya Ushirika kiuchumi, Vyama vya kifedha (SACCOS) vyenye mitaji imara.

Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi, Prof. Alred Sife katika hotuba yake iliyosomwa na Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi, Taaluma, Prof. John Safari, amesema ni matarajio ya Chuo kuwa, Makongamano ya Tafiti za Ushirika yatasaidia kuongeza uelewa wa vikwazo vya maendeleo ya Ushirika, Kujenga Ushirika unaoendana na mabadiliko ya kijamii na kiuchumi na kufanya Sekta ya Ushirika kuwa msingi imara wa Uchumi wa Taifa nchini.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Prof. Sizya Tumbo akiongea wakati wa akifungua rasmi Kongamano la kwanza la Tafiti za Ushirika linalofanyika katika ukumbi wa PSSSF Jijini Dodoma Machi 16, 2021 




Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Dkt. Benson Ndiege akieleza masuala ya Ushirika wakati wa Ufunguzi wa Kongamano la Tafiti za Ushirika Jijini Dodoma 

Mgeni rasmi Naibu Katibu Mkuu Prof. Sizya Tumbo akiwa amekaa (katikati) pamoja na viongozi wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika, Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi pamoja na Menejimenti ya Tume ya Maendeleo ya Ushirika wakati wa Kongamano la Tafiti za Ushirika

Post a Comment

Previous Post Next Post