Na John Mapepele, Dodoma
Tanzania imeandika historia ya kuwa na Rais mwanamke wa kwanza kwenye nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki ambapo Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ameapishwa rasmi tarehe 19 Machi, 2021 kushika wadhifa huo kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa Tanzania Hayati Mhe, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kilichotokea tarehe 17 Machi, 2021.
Kwa Mujibu wa ibara ya 37(5) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano, endapo kiti cha Rais kitakuwa wazi kutokana na Rais kufariki dunia, kijiuzulu, kupoteza sifa za uchaguzi au kutomudu kazi zake kutokana namaradhi ya mwili au kushindwa kutekeleza kazi za rais, basi Makamu wa Rais ataapishwa na atakuwa Rais kwa muda uliobaki katika kipindi cha miaka mitano.
Mara baada ya kula kiapo Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan akiwa na majonzi mazito amezungumza kwa kifupi na kuanza kwa kutoa ratiba ya mazishi ya mwili wa aliyekuwa Rais, Mhe. John Pombe ambapo amesema kutakuwa na vituo vinne (Dar es Salaam, Dodoma, Mwanza na Chato) vitakavyotumika kwa ajili ya kuagia ili wananchi wengi waweze kutoa heshima zao za mwisho kwa mpendwa wao katika kipindi hiki kabla ya mazishi rasmi tarehe 25 Machi 2021.
“Leo si siku nzuri ya kwangu kusema, kutokana na kidonda kikubwa moyoni na mzigo mzito nilionao. Nimekula kiapo katika mazingira tofauti, nimezoea kula kiapo katika mazingira tofauti, nimezoea kula kiapo katika hali ya nderemo na furaha lakini leo nimekula kiapo katika hali ya huzuni na masikitiko” amesisitiza Rais Samia Suluhu Hassan
Kama ilivyotarajiwa na watanzania wengi kuhitaji faraja na matumaini kutoka kwa Rais huyu mpya baada ya wimbi jeusi lililotanda ghafla baada ya jemedari na shujaa mwanamapinduzi Dkt JPM kuanguka, ndivyo ilivyokuwa baada ya Rais Samia kusoma hotuba yake fupi iliyosheheni mwanga wa matumaini mapya kwa Taifa iliyosisitiza upendo, mshikamano na umoja kwenye kipindi hiki cha maombolezo.
“Katika kipindi hiki cha maombolezo, ni kipindi cha kuzika tofauti zetu, huu ni wakati wa kuwa wamoja, huu si wakati wa kutazama yaliyopita, huu si wakati wa kunyosheana vidole bali huu ni wakati wa kutazama mbele kwa matumaini na kuweka mbele nguvu kwa pamoja ili kujenga Tanzania ambayo Mheshimiwa Magufuli aliitamani, na zaidi sana tuungane kumwombea (hayati John Pombe Joseph Magufuli) alale pema peponi.” Amefafanua
Waziri Mkuu Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Samwel Malecela amesema Taifa linapitia katika kipindi kigumu jambo la muhimu ni kuendelea kushikamana kama watanzania ili kupita kwenye kipindi hiki kwa umoja na upendo.
Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Julius Mtatiro anaona kuwa pamoja na kuondokewa na Jemedari Mkuu hayati Dkt. John Pombe Magufuli Mungu ataivusha nchi yetu itaendelea kuwa imara.
“Taifa hili ni imara,Mungu amelipendelea sana, halikuwahi kuyumba wala kutetereka katika nyakati zote za changamoto; yalipotokea maasi ya kijeshi mwaka 1964, alipofariki Mzee Karume mwaka 1972, nyakati mbaya za njaa, nzige na vita ya Uganda miaka ya 1970 na 1980, alipofariki Waziri Mkuu, Edward Moringe Sokoine mwaka 1984 na alipong’atuka madarakani na kufariki Muasisi na Baba wa taifa letu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Tusiogope na tusitetereke, sisi ni taifa imara siku zote,nyakati zote” anaongeza Mtaturu.
Rais Samia ameyashukuru makundi ya watu mbalimbali kwa kuendelea kushikamana na Serikali yake, makundi hayo ni pamoja na Chama cha Mapinduzi,viongozi wakuu wastaafu, vyombo vyote vya ulinzi na usalama na viongozi wa dini.
Pia kwa namna ya pekee amewashukuru Wasanii na Waandishi wa Habari kwa kuendelea kutumia taaluma zao katika kuwaunganisha watanzania kuwa kitu kimmoja wakati wote. Baadhi ya Wasanii wakongwe wa muziki na Waandishi wameonekana kuguswa sana na hotuba hii na kutoa ya moyoni:
“OOOh, No. ungekuwepo wakati tunaangalia hii hotuba ilibidi tukae tuangalie kwenye luninga, mimi binafsi nilikuwa ninanena kwa lugha nakumbuka nilikuwa nimezungukwa na vijana nikawamuru watulie kwa sababu huu ndiyo wakati wa bwana, nikawambia Mungu alipotaka kuwakomboa Taifa la Israel toka kwenye nchi ya utumwa alimtumia mwanamke na kwamba aliweka hekima ndani ya mwanamke na wakati huu Mungu ameweka mwanamke kwa maana kuna jambo ambalo Mungu anataka kutuingiza” amesema Christina Shusho, mmoja wa waimbaji wakongwe wa nyimbo za Injili hapa nchini.
“Mimi napenda kwenda na neno la kinabii Mheshimiwa Rais Samia ametuheshimisha sana wasanii wa Tanzania maana kuna makundi mengi lakini sisi wasanii tumependelewa tumetajwa katika hotuba ya kwanza natambua makundi mengine yataendelea kutajwa” ameongeza Shusho.
Kuhusu kifo cha Dkt. Magufuli Shusho amesema hayati Rais Magufuli hakuona haya kumtambulisha Mungu wake katika kila hatua aliyopita pamoja na nafasi aliyokuwa nayo:
” kuna watu ambao tunampenda Mungu tunamjua Mungu tunapokuwa chini, tukiinuliwa hivi kama mimi wa bwana Yesu asifiwe unakuta vinapungua kwa sababu ya position niliyoipata lakini Mheshimiwa Rais JPM hakumwacha kumsema Mungu wake wakati yeye ndiye alikuwa kiongozi Mkuu namba moja katika nchi yetu”.
Mwanamuziki Nguli nchni, Mrisho Mpoto amesema Wasanii na Wanamuziki wataendelea kumkumbuka Dkt. Magufuli kwa kuwa hakuwabagua, kila msanii alimfanya sawa na mwingine kiasi cha kumfanya kila msanii ajione anapendwa na Rais JPM.
“Utakumbuka mtindo wake wa kuwavisha kofia yake alijitahidi sana kwa kadiri alivyoweza kufanya hivyo kwa kila msanii, mimi binafsi aliwahi hata kunitambulisha kuwa ni mwanamuziki bora kabisa na yeye ni shabiki wangu na kwenda mbali zaidi kwa kuimba baadhi ya nyimbo zangu mbele ya umati wa watu” amesema Mpoto kwa furaha
Mwandishi wa Habari wa kujitegemea Dotto Mwaibale amesema falsafa ya Dkt. Magufuli ya kuenzi lugha ya Kiswahili duniani umewafanya hata Viongozi wakuu barani afrika kufikiria kuanza Kiswahili kama lugha rasmi katika nchi hizo.
Mwandishi wa Makala haya ni Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini kwenye Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo anapatikana katika: jmapepele1@ gmail.com au 0784441180