PROF. OLE GABRIEL AMNASA ALIYEKUA AKIJARIBU KUKWEPA UTARATIBU WA KUSAFIRISHA MIFUGO

 Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia idara zake za Uzalishaji na Masoko na ile ya Huduma za Mifugo kwa kushirikiana na jeshi la Polisi wamefanikiwa kumkamata Mfanyabiashara wa mifugo Bw. Joseph Bonifasi ambaye alikuwa anasafirisha Ng’ombe kuelekea mkoani Lindi kinyume na taratibu.


Tukio hilo limetokea Usiku wa Kuamkia leo (11.03.2021) katika kizuizi kilichopo eneo la Mbande jijini Dodoma ambapo Polisi walizuia gari iliyobeba ng’ombe hao na kumkamata mmiliki wake baada ya kuzitilia mashaka nyaraka zilizotumika kuwasafirishia.

“Baada ya kumkamata, alikataa kufuata taratibu zinazotakiwa na badala yake akampigia simu Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel na kwa kweli tunamshukuru sana Katibu Mkuu kwa sababu tofauti na alivyodhani mtuhumiwa wetu, yeye aliamuru ashikiliwe mpaka watendaji wa Wizara watakapofika hapo na kujiridhisha juu ya uhalali wa nyaraka hizo” Alisema mmoja wa Askari aliyekuwepo kwenye kizuizi hicho.

Muda mfupi baada ya kufika katika eneo la tukio, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Uzalishaji na Masoko Bw. Stephen Michael akiwa ameambatana na timu ya wataalam kutoka idara ya huduma za mifugo walikagua nyaraka hizo na kubaini dosari kadhaa ikiwemo kuisha kwa muda wa matumizi wa kibali kilichotumika kusafirishia mifugo hiyo.

“Lakini pia tumebaini kuwa kibali hiki kimetumika kusafirishia mifugo zaidi ya mara moja ambapo kimeonekana awali kilitumika kusafirishia mifugo mingine kutoka Tura kwenda Pugu kabla ya kutumika tena kusafirishia ng’ombe kwenda Mtwara kupitia Manyara, Dodoma, Morogoro na Pwani na mbaya zaidi taarifa za awali zimekatwa na kuandikwa nyingine kwa juu” Amesema Stephen.

Mbali na dosari zilizoonekana kwenye nyaraka za kusafirishia ng’ombe hao, Mfanyabiashara huyo pia amefanya kosa la kusafirisha ng’ombe wakubwa na watoto (ndama) kwa wakati mmoja kinyume na sheria ya haki za wanyama ya mwaka 2010 ambayo kipengele cha 8 (1) kinachohusu usafirishaji  ambacho kinaainisha kuwa mhusika ni lazima azingatie uzito,ukubwa na maumbo ya ng’ombe kabla ya kuwasafirisha kwa pamoja.

Kwa upande wake Mfanyabiashara huyo alikiri kufanya kosa la kutokuwa na nyaraka halali za kusafirishia ng’ombe hao ambapo pia alitoa wito kwa wafanyabiashara wenzake kutii sheria wakati wote wanapopaswa kufanya hivyo.

“Nitakuwa balozi mzuri kwa wenzangu na kuanzia sasa hata nikiona mfanyabiashara mwenzangu hajafuata taratibu za kusafirisha mifugo yake, ntakuwa wa kwanza kuripoti kwenye mamlaka husika” Amesema Bonifasi.

Hivi karibuni Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia sekta ya Mifugo iliunda kikosi kazi maalum kwa ajili ya kufanya doria ya kudhibiti utoroshwaji wa mifugo mipakani na kwenye vizuizi mbalimbali zoezi ambalo tayari limeshaonekana kuanza kuzaa matunda.



Post a Comment

Previous Post Next Post